Mashairi

SOKOMOKO: Kila la heri wenzangu

April 6th, 2019 4 min read

MKUSANYIKO wa mashairi Jumamosi, Aprili 6, 2019.

Kila heri wenzangu

Elimu ndiyo maisha, kwetu sisi wanadamu,
Elimu huburudisha, akikufunza mwalimu,
Elimu hutufikisha, pahali tusofahamu,
Kila la heri wenzangu, kutoka Chuo cha Moi,

Maisha yote chuoni, mengi mmevumilia,
Ya furaha na huzuni, kweli mmejionea,
Japo kweli masomoni, hamkukata tamaa,
Kwa wenu uvumilivu, Mungu awapiganie.

Kwa wanafunzi wengine, wanaofuzu shahada,
Hasa wa mwaka wa nne, msije ishi kwa shida,
Nafurahi mi nione, mnaishi bila shida,
Kila la heri Rebecca, dadangu kutoka Voi.

Baba Mungu wa mbinguni, kazi awafungulie,
Mnapofuzu chuoni, sitaki mkaumie,
Bali mkafurahini, na huru mjisikie,
Kutoka kwangu Hosea, kila la heri wenzangu.

HOSEA NAMACHANJA
Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret

 

Umri umetimia, dalili sioni

Yanitia wasiwasi, je mwanangu ana mume?
Nenda wewe mdadisi, fanya siri ayateme,
Jirani mpe notisi, mdadisi usikome,
Umri keshatimia, dalili sioni mie.

Mrembo kama tausi, tabia zake kiume,
Mwadilifu si kitasi, kwangu mi kama mtume,
Makini uwe kijusi, akupe jina la ndume,
Umri keshatimia, dalili sioni mie.

Hapendi yule mbesi, hata nao gumegume,
Hataki wenye mikosi, huwatema walo shume,
Jirani nenda uakisi, atengeani waume?
Umri keshatimia, dalili sioni mie.

Yeye hupenda kuasi, hajayaona ukame,
Anyaukapo ni kesi, watasusa wanaume,
Kaditama wasiwasi, nayotongoa siseme,
Umri keshatimia, dalili sioni mie.

GLADYS KIRISWO
‘Toto Shombe’
Eldama Ravine

 

Heri nife jehanamu

Utumwa sitakubali, mwana ninatia nanga,
Ya mbeleni sitojali, ndimi Kuku wa Zabanga,
Unafiki ubadili, ama nije kwa upanga,
Sitakubali utumwa, heri nife jehanamu.

Utumwa sitakubali, nichapeni mkitaka,
Nitie adhabu kali, mnitoe na sadaka,
Tabia sitobadili, niueni ntajizika,
Sitakubali utumwa, heri nife jehanamu.

Heri nife jehanamu, kwenye moto wa milele,
Vya mbinguni tamutamu, nivikose nisivile,
Nibaki kujilaumu, niziepuke kelele,
Sitakubali utumwa, heri nife jehanamu.

Utumwa sitakubali, hata mama yuajua,
Sheriaze kalikali, zilipita na mvua,
Kabla kufa kaka Neli, vyema angekuambua,
Sitakubali utumwa, heri nife jehanamu.

GILBERT KINARA
‘Mwamba wa Keumbu’
Keumbu, Kisii

 

Wasanii njooni

Nawaita wasanii, njooni sana haraka,
Mje muione hii, ibura iliyozuka,
Kwa mimi hainiwii, rahisi kueleweka,
Aloita aitika, muitwa haitikii.

Walikuja manabii, na kisha wakaondoka,
Hakuna aliyetii, yale waliyotamka,
Vyereje kwa leo hii, tumebakia kumaka,
Chalia kilopigika, anayepigwa halii.

Mashekhena mawalii, hapa wamekusanyika,
Zimewaisha bidii, za kutaka kweleweka,
Hivi wamebaki zii, macho yamewatumbuka,
Wasikia wasotaka, aambwaye hasikii.

MOHAMMED SHABAN ALI
Mpembuzi/Matishali
Ganjoni

 

Miti raslimali kubwa

Ushukuriwe Rabana, kwa kutujali Jalali,
Uinuliwe bayana, kwa kuiumba aali,
Uliumba loamana, viumbe vinotujali,
Miti ni rasilimali, naomba tuithamini.

Naomba nisikieni, nataka kuligusia,
Hino hoja natamani, itambe kote dunia,
Walokiuka kanuni, wasije wakajutia,
Miti ni rasilimali, naomba tuithamini.

Hutupatia mvua, majiyo tunatumia,
Hulinda vyanzo jua, maji sijekaukia,
Uweze tena ng’amua, momonyoko huzuia,
Miti ni rasilimali, naomba tuithamini.

Malighafi imetupa, kazizo zaonekana,
Mifano pale na hapa, samani zipo waona,
Madawa yapo naapa, yanotibu nakupona,
Miti ni rasilimali, naomba tuithamini.

TONEY FRANCIS ONDELO
‘Chomsky Mswahili’
‘Malenga Mjali Siha’
Ndhiwa

 

Mazingira ngao yetu

Swahibu nawasalimu, mu hali gani jamani?
Nimeona ni muhimu, yangu kuwajuvyeni,
Nitaamba ya kudumu, kwani sisi tu tabani,
Mazingira ngao yetu, kuharibu tutajuta.

Yamekuwa ya kudumu, tangu zamani nchini,
Kashika yake hatamu, yakafika kileleni,
Kasifiwa humu humu, Maathai duniani,
Mazingira ngao yetu, kuharibu tutajuta.

Imegeuka awamu, sasa kote hatarini,
Tuloyasifu mfahamu, yamegeuka jangani,
Kulia mewa vigumu, kubadili hili yani,
Mazingira ngao yetu, kuharibu tutajuta.

Tatizo uchakaramu, wa kukata misituni,
Kielezwa ndiyo sumu, hamnazo mwapatani,
Hamtaki kufahamu, mazingira bora yani,
Mazingira ngao yetu, kuharibu tutajuta.

PETER WANJOHI
‘Kitungu Machoni’
Narok

 

Waridi nitazidi kuvutia

Ua tamu la waridi, yakini sitanyauka,
Na tena ninaahidi, kuzidi kuimarika,
Kwa uvumba kwa udi, niwe ni wa kupendeka,
Waridi mie waridi, nitazidi kuvutia.

Kwa kweli nitapendeza, huku Bara hadi Pwani,
Rangi nitaikoleza, nilipiku asumini,
Ninakana kuchukiza, bali tavutia mboni,
Waridi mie waridi, nitazidi kuvutia.

Vipepeo hadi nyuni, wote nitawapendeza,
Watapepea angani, kisha kwangu wakacheza,
Pia midege tunduni, wote watajitokeza,
Waridi mie waridi, nitazidi kuvutia.

Tamati hapa tamati, kutamati sina budi,
Rangi yangu chokoleti, yavutia auladi,
Naipiku alizeti, ajua hilo Wahidi,
Waridi mie waridi, nitazidi kuvutia.

MERCY NOREY
Nakuru

 

Ukienda haurudi

Shairi ninakutuma, umfikie Nyamai,
Ukaseme kwa heshima, hivi leo ajidai,
Ni sikuye ilo njema, tunywe soda sio chai,
Ujana kweli ni moshi, ukinenda haurudi.

Siku yake kuzaliwa, aingia ukubwani,
Naomba aje jaliwa, siha yake siwe duni,
Na asiwe na shakawa, aishipo duniani,
Ujana kweli ni moshi, ukinenda haurudi.

Mwenzake mie Aseli, ninamtakia mema,
Aushini asifeli, kwa huzuni akazama,
Fanaka ya kila hali, akapate himahima,
Ujana kweli ni moshi, ukinenda haurudi.

Umweleze sikioni, hili jambo la adhama,
Akaseme shukurani, kwa babake pia mama,
Walomkuza nyumbani, awe binti wa heshima,
Ujana kweli ni moshi, ukinenda haurudi.

BOAZ ASELI
Ustadh Kipepeo

 

Tanuri lakungoja

Tenda tenda mwanangu, tenda wala usihofu,
Nakwambia kwa machungu, sitende laanifu,
Sikupi mie mapingu, wewe tenda maumbufu,
Yatende mwanangu, tanuri lako lawashwa!

Chuchu zako sifunike, ziwachie hewa mwana,
Wacha jua limulike, wazione kwa upana,
Kwani wewe si ni mke, nani tena atakana?
Waonyeshe hizo chuchu, wazione kwa hiari.

Makalio yanengue, yapwaishe kweli kweli,
Fanya macho wafungue, kuduwaa kwa kejeli,
Ni machizi wazingue, wakufuate mwanamwali,
Fanya hayo ukingoja, moto wako utafika.

Vipodozi pangilia, uso wote ukumete,
Rangi zote kimbilia, wewe mwana si kiwete,
Kucha gushi dungilia, ulimbwende upakate,
Endelea na mitindo, moto uje uchomeke!

AGGREY BARASA
‘Bongopevu’
MMUST, Kakamega

 

Elimu izingatie

Nakukumbusha, ushike wangu wasiya,
Dunia yawashawasha, michomo ya kila njiya,
Ugumu wayo maisha, ni bora kunyenyekeya,
Mwanangu nakuusiya, elimu izingatie.

Mengi tumekufundisha, ufaidike sikiya,
Ili uje kujivusha, dunia twatarajiya,
Kwa kuwa inawatisha, hata walo na rupiya,
Mwanangu nakuusiya, elimu izingatie.

Ujuwe havitoisha, vishawishi kukujiya,
Na hodi havitobisha, ghafula vitafikiya,
Walimwengu hupotosha, mja akadidimiya,
Mwanangu nakuusiya, elimu izingatie.

Na waovu jiepusha, chuoni ukifikiya,
Wao watakuyumbisha, yale ulodhamiriya,
Tama watakuzamisha, dimbwi la hino duniya,
Mwanangu nakuusiya, elimu izingatie.

MAINAH ALFRED MAINAH
Mia moja, Timau

 

Moyo wangu wayeyuka

Mahali hapa nilipo, nimejawa majonzi,
Popote wewe ulipo, nimechoka na machozi,
Unapepea ja popo, mi sipati usingizi,
Moyo wangu wayeyuka, fuadi inafifia.

Akilini ungalipo, moyoni umeniganda,
Umekuwa kama pepo, mwili wangu unakonda,
Nakumanya na haupo, kazi yako ni kuwinda,
Moyo wangu wayeyuka, fuadi inafifia.

Wakumbuka ulosema, ahadi zako ni feki,
Nikakupa na heshima, kakulisha pia keki,
Ukashindwa na kukoma, ukazoa kama reki,
Moyo wangu wayeyuka, fuadi inafifia.

Usingizi menikaba, imebidi nikalale,
Nimechoka na si haba, yananisonga ya kale,
Machungu yamenikaba, natamani nikayale,
Moyo wangu wayeyuka, fuadi inafifia.

DUNNETA SAMAMA
‘Malenga wa Mashinani’
Awendo, Migori

 

Jameni samehea

Haikuwa nia yangu, mi kukosea,
Ni udhaifu wangu, lilokuwa mekolea,
Siyo kupenda kwangu, mwenzako kukosea,
Huu udhaifu wangu, jamani samehea.

Binadamu huudhi, pia hukasirisha,
Nisikulete maradhi, jamani samehesha,
Msamaha ya hadhi, moyo hufurahisha,
Huu udhaifu wangu, jamani samehea.

Asante nikubaliya, msamaha nikuombe,
Kulisoma shairiya, msamaha si kikombe,
Upendo huashiriya, msamaha so pombe,
Huu udhaifu wangu, jamani samehea.

CORNELIUS WANJOYA
Sigalagala, Kakamega