Mashairi

SOKOMOKO: Mtu ni utu

June 22nd, 2019 5 min read

NAANZA kwa la Jalia, jina lenye utukufu,

Kofia nawavulia, nawapa heko sufufu,

Mioyo naisifia, yenu iso usumbufu,

Mtu ni mwenye utu, aso utu ni jeraha.

 

Nyoyo nzuri nasifia, zisizo na mapungufu,

Nyoyo zilotulia, zisizo na maumbufu,

Maisha kuteremea, ukaishi bila hofu,

Mtu ni mwenye utu, aso utu ni jeraha.

 

Tamati imetimia, twaomba ukamilifu,

Matunda tajivunia, kutoka kwa Mtukufu,

Mema yakitutokea, ni aali kuyasifu,

Mtu ni mwenye utu, aso utu ni jeraha.

IBRAHIM SIMIYU

‘Yakuti Msi Kilemba’

 

Mja hakosi kasoro

Chokoraa wasemavyo, maskani mitaani,

Kuombaomba tulivyo, majukumu maishani,

Tukupanga ishi hivyo, twateseka aushini,

Ombi nyie mtujali, mja hakosi kasoro.

 

Mwasema twala pipani, ‘gonjwa nadra mwilini,

Nyie hospitalini, wataalamu ya nini,

Upendo mlithamini, tujali barabarani,

Ombi nyie mtujali, mja hakosi kasoro.

 

Maisha yetu magumu, mithili mbwa twaishi,

Kisingizio wazimu, midomoni hayaishi,

Kwa Jalali ni haramu, watunyima pia keshi,

Ombi nyie mtujali, mja hakosi kasoro.

 

Tushikanapo imara, amani hupatikana,

Wachache waja hongera, ni nyingi kwetu thamana,

Rohoni mweupe dura, azidishe Maulana,

Ombi nyie mtujali, mja hakosi kasoro.

LEXY SON BREVYN

‘Kiamboni Ustadh’

Nzoia Academy, Kitale

 

Uovu umezidi

Iwapo angefufuka, Rolihlahla muadhama,

Mzee angegutuka abaki akiachama,

Mtima ungeatuka imwondoke naima.

Nyuma angekukumbuka, za mkoloni dhuluma.

 

Raia walivyoteka, wengine wakiwachoma,

Moyoni angesumbuka, abaki kushika tama.

Suduri ingepasuka, angesikia tuhuma,

Kilio cha Afrika, Kusini kumezizima.

 

Wanaua wakibaka, kwa mishale wakifuma.

Angeomba kwa Rabuka, Kusini isije zama,

Wauache utabaka, na rangi kutizama,

Kwani jino liking’oka, uso wote hutetema.

MOSES CHESIRE

‘Sumu ya Waridi’

Kitale

 

Rabbi tupe faraja

Haya mambo ni kangaja, ninalisuka kombeo,

Dua niombe faraja, tuziepuke dhurio,

Binadamu kupembeja, kifilisi matukio,

Yarabi tupe mafao, utukidhi zetu haja.

 

Wananchi tumengoja, kwa hamu wetu mgao,

Tupate nasi kuoja, nchini maendeleo,

Barabara madaraja, tusafirishe mazao,

Yarabi tupe mafao, utukidhi zetu haja.

 

Viongozi kwa pamoja, wala njama kwa vikao,

Na nia mbaya harija, wazijaze tumbo zao,

Njaa imetubigija, wao wala na salio,

Yarabi tupe mafao, utumishi zetu haja.

 

Mwisho naomba faraja, watu kwa yao makao,

Mali ya umma kufuja, wasifanye watu hao,

Tuvionavyo vioja, viwe mwisho matukio,

Yarabi tupe mafao, utukidhi zetu haja.

MAINAH ALFRED MAINAH

‘Msanifu Makamula’

Mia Moja, Timau

 

Mashangingi mna mambo

Mashangi wanabobea, wako nao mchezoni,

Waume kuwakwachua, si Juma si Kaloleni,

Wenye sawa jinsia, husalia kilioni,

Mashangingi mna mambo, waume mwamaliza.

 

Mashangingi kukwatua, habatishi kaulini,

Wajihi kaupodoa, mithili hurulaini,

Kanga wamejifungia, walezi kule nyumbani,

Mashangingi mna mambo, waume mwamaliza.

 

Mashangingi hunyakua, sababu nzuri lisani,

Kifua kujilazia, mara bebi mara hani,

Wa kwake kumfokea, sasa mume anafani,

Mashangingi mna mambo, waume mwamaliza.

 

Mashangingi huvutia, waume huwatamani,

Mapenzi hukusudia, na msukumo mapeni,

Wake huwakumbatia, wenza kiwa mwezini,

Mashangingi mna mambo, waume mwamaliza.

GLADYS KIRISWO

‘Toto Shombe’

Eldama Ravine

 

Viongozi wanaisha

Kaondoka Muhamadi, Morsi wa Kimisri,

Mushituko wa fuadi, kaagana na sayari,

Kamtwalia Wadudi, kumwondolea ghururi,

Majuto huja kwa dhiki, Waafrika tuzinduke.

 

Sina nia ya kulia, kukashifu ndiyo nia,

Maudhia kuwambia, Waafrika kusikia,

Fikira twajifumbia, Wazungu kuwasikia,

Majuto huja kwa dhiki, Waafrika tuzinduke.

 

Nianze taja Gaddafi, jenerali Mwafrika,

Maonoye liwa safi, wenyewe tukampoka,

Kwa mawazo ya kighafi, ya wazungu vibaraka,

Majuto huja kwa dhiki, waafrika tuzinduke.

 

Twawauwa viongozi, kwa hadaa na tuhuma,

Kutajia kwa baadhi, Iddi ni mfano mwema,

Uganda wake wongozi, udikteta utakoma?

Majuto huja kwa dhiki, Waafrika tuzinduke.

RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE

‘Malenga Wa Nchi Kavu’

 

Mbona ulinitupa

Mama mzazi hujambo, mwanao nakusalimu,

Mie binafsi sijambo, nakwarifu ufahamu,

Yepi liyojiri mambo, katika hii awamu,

Mbona mama linitupa, niarifu nikamanye.

 

Mwanao nakuuliza, nileze kinaganaga,

Mie kindako nawaza, mtotowe kunibwaga,

Mbona ulinibwagaza, na kuniachia woga,

Mbona mama linitupa, niarifu nikamanye.

 

Kujikaza najaribu, bila zako shukrani,

Makuzo bila abu,kila mara matesoni,

Kila wakati adhabu, malezi pasi amani,

Mbona mama linitupa, niarifu nikamanye.

 

Nairobi ulikwenda, nyuma ukanisahau,

Nikaandamwa na chonda, moyo kakosa ubuu,

Nikawa pasi na funda, nikapata nyingi dharau,

Mbona mama linitupa, niarifu nikamanye.

VINCENT OKWETSO

‘Malenga Chipukizi’

MMUST, Kakamega

 

Sikati tamaa

Ndio ni watu kadhaa, wenyewe wanajijua,

Wananiombea baa, nyota yangu kuchafua,

Ili iwache kung’aa, kama ling’aavyo Jua.

Sasa ninayo dhiyaa, imetimu yao dua,

 

Kila uchao balaa, dhiki zinanisumbua,

Njiani ninajikwaa, bila hata kutambua.

Ila sikati tamaa, midhali ninapumua,

Kinyonga tini kukaa, haiwi haitakua,

 

Ijapo kwa kutambaa, nitaivuta hatua.

Sitabaki kushangaa, sasa ninajinyanyua,

Wapae wenye kupaa, ila nao nitatua,

Wabakiwe na butwaa, mato wakiyatumbua.

 

Tama sitakufa njaa, hili vema wakajua,

Tusi waliloandaa, na sanda walonunua,

Zitaenda kuchakaa, Mola keshaninasua.

DOTTO RANGIMOTO

‘Jini Kinyonga’

Morogoro, Tanzania

 

Ndoa za mapema

Ni habari zachukiza, kwa moto kutopuliza,

Watu pia kupumpaza, hakuna wa kusikiza,

Leo hili nalipaza, binti dogo kumuoza,

Ndoa hizi za mapema, binti mdogo zamtweza.

 

Ana haki yeye pia, maishani kuchupia,

Kamtunuku Jalia, binti huyu maridhia,

Ajihisi ni insia, asabilie dunia,

Ndoa hizi za mapema, binti mdogo zamtweza.

 

Ndoto na matumaini, anazo hima yakini,

Apitie masomoni, hadi hata vyuoni,

Asichekwe ndiani, matusi nazo laani,

Ndoa hizi za mapema, binti mdogo zamtweza.

 

Muhimu wake umuri, afikie mwanamari,

Kuanza hizo safari, zakuonyesha uzuri,

Kumuoza ni hatari, bila mwili hariri,

Ndoa hizi za mapema, binti mdogo zamtweza.

KHALID ABDIRAZAK

‘Mwana wa Jangwani’

Garissa

 

Ubwana na utwana

Miye nikitafakuri, fikira kuzungulusha,

N’jiuliza hii siri, ya mfumo wa maisha,

Nawe hili ufikiri, kisha utanijulisha,

Ya ubwana na utwana, kweli yameshatoweka?

 

Yale yalobadilika, n’fikiri ni matamshi,

Yule anayetumika, akiitwa mtumishi,

Na mwajiri uhakika, kuwa bwana haiishi,

Ya ubwana na utwana, kweli yameshatoweka?

 

Si bora kwitwa mtwana, huku nimeshiba sana,

Bosi n’kamuita bwana, tukiwa tumeshibana?

Utumishi naukana, unaoninyonya sana,

Ya ubwana na utwana, kweli yameshatoweka?

 

Wasanii washairi, nyie mtanieleza,

Hili mlitafakari, mujibu kina Kaliza,

Kissamvu nawe Sheeri, na wengine nawauza,

Ya ubwana na utwana, kweli yameshatoweka?

RWAKARWA KAGARAMA

‘Mshairi Mnyarwanda’

Nyagatare, Rwanda

 

Mimi ni ganda la ndizi

Nakuchamba wima wima, mgeni sitaki kiti,

Sura ka mbuzi ya homa, ng’ombe ulokosa titi,

Nikome mwana wa Mama, nitakupiga mashoti,

Mimi ni Ganda la ndizi, chunga usinikanyage.

 

Wewe jini la chooni, mimi jini la bahari,

Ajaye anakulani, hutakiwi hata heri,

Umenifika kooni, Leo sitakusitiri,

Mimi ni Ganda la ndizi, chunga usinikanyage.

 

Huyo uliyemtuma, hukumlipa vizuri,

Alikuja na huruma, kunipa nyingi habari,

Kumbe nikipata nema, wakesha kwenye ndunguri,

Mimi ni Ganda la ndizi, chunga usinikanyage.

ABDULKARIM KUCHENGWA

 

Zawadi bora kakangu

Leo ndio siku yako, uliozawa hakika,

Siku bora kwa mamako, na wengine kadhalika,

Furaha navyo vicheko, vilitanda huo mwaka,

Zawadi bora kakangu, mshukuru Mola wako.

 

Ulisumbua nduguzo, ulipokua kidaka,

Ulikuwa na mauzo, kila moja akutaka,

Ni matunzo mzomzo, wazazi waliyaweka,

Zawadi bora kakangu, mshukuru Mola wako.

 

Masomo uliyapata, ya chuo na sekondari,

Elimu nyingi mepata, usijione hodari,

Heshima umeshapata, wewe kwetu ni jabari,

Zawadi bora kakangu, mshukuru Mola wako.

 

Twakuamini kwa kazi, ya kucheza na kamera,

Kuediti kwako kazi, si ukunda si Kibera,

Watambua kwa ujuzi, na una nyingi fikira,

Zawadi bora kakangu, mshukuru Mola wako.

BAKARI MWAKUZIMU

‘Malenga Wa Ufukweni’

Kwale

 

Mama niombee dua

Mama niombee dua, nakuomba kwa hisani,

Ahsante kunikopoa, kunileta duniani,

Malezi kunipatia, masomo kutonihini.

Mama niombee dua, udumu mwangu moyoni.

 

Niswafiye yako nia, pendo lizidi thamani,

Ya kwangu yawe murua, ipunguwe mitihani.

Mama niombee dua, nizikumbuke ihsani,

Yote ulonitendea, niyatie akilini.

 

Nisiwahi kukosea, kesho nikenda motoni.

Mama niombee dua, nisimfwate shetwani,

Niwe na njema tabia, nizingatie ya dini,

Nisiende piapia, kujitia madhambini.

 

Mama niombee dua, niwe na siha mwilini,

Afiya kunikolea, niwe timamu kichwani,

Heshima kushikilia, hekima iweko ndani.

BAMSULEY ABDALLAH

‘N’nge Mpole Mshairi Kinda’