Michezo

Sokratis aomba msamaha baada ya Arsenal kula sare

September 17th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

ILIMLAZIMU beki Sokratis Papastathopoulos kuomba msamaha ili kutuliza hasira za mashabiki wa Arsenal waliomchemkia kwa kosa lililowapa Watford fursa ya kurejea mchezoni na hatimaye kusajili sare ya 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyochezewa ugani Vicarage Road wikendi iliyopita.

Sokratis mwenye umri wa miaka 31 alisema kwamba ndiye aliyestahili kulaumiwa kwa matokeo hayo yaliyowanyima Arsenal fursa ya kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali.

Pierre-Emerick Aubameyang aliwafungia Arsenal mabao mawili kabla ya masihara ya Sokratis kwenye safu ya nyuma kuwapa Watford bao muhimu lililowarejesha mchezoni katika kipindi cha pili.

Difenda huyo mzawa wa Ugiriki alikuwa akijaribu kupiga pasi fupi kuelekea katikati ya uwanja baada ya kupokezwa mpira na kipa Bernd Leno kabla ya mvamizi Gerard Deulofeu kuuwahi na kumpa krosi kiungo Tom Cleverley aliyecheka na lango la wageni wao.

Mwishoni mwa kipindi cha pili, Roberto Pereyra aliwafungia Watford bao la pili kupitia mkwaju wa penalti baada ya kiungo huyo kukabiliwa visivyo na beki David Luiz ndani ya msambamba.

Mwishoni mwa mechi hiyo, Sokratis aliandika ujumbe wa msamaha na kupakia kwenye ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa Twitter ili uwafikie zaidi ya wafuasi wake 86,700.

“Nahisi kuhukumika baada ya matokeo ya mchuano. Ndiye ninayestahili kulaumiwa kwa ubovu wa matokeo haya. Hivyo, naomba msamaha kutoka kwenu nyote. Nisingependa kuficha hisia zangu, ila naapa kujitahidi zaidi ili kuweka hai tumaini la kuyafikia malengo yetu,” akaandika beki huyo.

Juhudi za kujinyanyua

Arsenal wanatarajiwa kujinyanyua mnamo Alhamisi watakaposhuka dimbani kumenyana na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani katika kivumbi cha ufunguzi wa Europa League.

Watakuwa baadaye wenyeji wa Aston Villa uwanjani Emirates mnamo Jumapili, siku moja baada ya Watford kuwaendea mabingwa watetezi wa taji la EPL, Manchester City ugani Etihad.

Kwa upande wake, nahodha na kiungo wa Arsenal Granit Xhaka alisema kwamba kikosi chao kilishuka dimbani kuvaana na Watford kikiwa na uoga tele hasa baada ya kuteleza katika mechi zote za mikondo miwili msimu uliopita.

Watford walilenga shabaha kwenye lango la Arsenal mara 31 huku 23 kati ya mipira hiyo iliyopanguliwa na kipa Leno ikichanjwa katika kipindi cha pili.

“Hakuna aliyetaka kupokezwa mpira kwa wakati fulani, ili asije akapoteza alaumiwe na wenzake. Hatukucheza jinsi ilivyotarajiwa na wengi hasa katika kipindi cha pili,” akasema Xhaka.

Tangu mwanzo wa kampeni za EPL msimu huu, Arsenal wamefanya jumla ya makossa 14 ambayo yamechangia mabao kwa upande wa wapinzani wao. Makombora 31 ambayo Arsenal walielekezewa langoni pao ndiyo idadi kubwa zaidi kwa Arsenal kuwahi kushuhudia katika kivumbi cha EPL tangu 2003-04.

Baada ya kusajili ushindi katika michuano miwili ya ufunguzi wa msimu huu dhidi ya Newcastle United na Burnley, Arsenal kwa sasa wamepiga jumla ya mechi tatu bila ya ushindi hasa baada ya kukomolewa na Liverpool kisha kuambulia sare dhidi ya Tottenham Hotspur na Watford.