Habari

SOLAI: Serikali yaondoa maji katika mabwawa mengine mawili

May 11th, 2018 1 min read

Na ERIC MATARA

WAHANDISI wa serikali Ijumaa waliondoa maji yaliyokuwa katika mabwawa mengine mawili yaliyo karibu na bwawa la Patel, eneo la Solai lililoangamiza watu 44 Nakuru.

Wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Maji (Warma) walisema walichukua hatua hiyo ili kuzuia mkasa mwingine kama huo kutokea kighafla.

Mojawapo ya mabwawa hayo mawili lilikuwa likipenyeza maji hapo Alhamisi jioni, hali iliyozua hofu ya kuvunja kingo zake na kuua watu zaidi.

Bwawa la Patel ni moja kati ya mabwawa matatu yanayomilikiwa na mwekezaji mtajika wa kilimo Patel Mansukul.

Mshirikishi wa eneo la Rift Valley Bw Mongo Chimwanga na mwenyekiti wa Warma Simon Wang’ombe waliongoza zoezi hilo lililosimamiwa na wahandisi kutoka serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Nakuru.

“Kundi la kiufundi la wahandisi lilikaugua mabwawa hayo Alhamisi jioni na kuwasilisha ripoti kwa mamlaka husika. Hapo Ijumaa maji yote katika mabwawa yaliondoloewa,” akasema Bw Chimwanga.

Hapo Alhamisi, iliibuka kuwa mabwawa yote katika eneo hilo hayakuwa na leseni ya ujenzi.

Warma ilijitetea kuwa imekuwa ikijaribu kuifikia kampuni ya Patel Coffee Estates Limited ili kuhalalisha bwawa hilo, lakini juhudi zao zimegonga mwamba.

Hii ni baada ya kung’amua hatari iliyokuwa ikiwakodolea macho wakazi walioishi upende wa chini wa bwawa hilo, walipoona maji yakipenyeza.

Meneja wa Warma eneo la Rift Valley, Simon Wang’ombe, alisema maafisa wake wamekuwa wakizuru eneo hilo mara kwa mara kukagua mabwawa.

Alifafanua kuwa sheria inasema kuwa bwawa la kibinafsi lenye urefu wa mita tano juu linahitajika kuhidhinishwa na shirika hilo.

“Kwa mwaka mmoja uliopita, tumekuwa tukijaribu kuwasiliana na maafisa wa kampuni hiyo bila mafanikio. Kulingana nasi, bwawa hili halikujengwa kulingana na sheria,” akasema.