Solskjaer amfuatilia Erling Braut Haaland kwa nia ya kumshawishi ajiunge na Manchester United

Solskjaer amfuatilia Erling Braut Haaland kwa nia ya kumshawishi ajiunge na Manchester United

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amesema kwamba anamfuatilia fowadi chipukizi wa Borussia Dortmund, Erling Braut Haaland ambaye ni raia mwenzake wa Norway kwa matumaini ya kumsajili mwishoni mwa msimu huu.

Solskjaer aliwahi kumnoa Haaland, 20, kambini mwa Molde ya Ligi Kuu ya Norway mnamo 2017 kabla ya chipukizi huyo matata kuhamia Austria kuvalia jezi za Red Bull Salzburg.

Tangu aingie kambini mwa Dortmund, Haaland amepachika wavuni jumla ya mabao 38 kutokana na mechi 40, ufanisi ambao umemfanya kuwa kivutio kambini mwa klabu nyingi barani Ulaya, ikiwemo Real Madrid ya Uhispania.

Katika mahojiano yake na gazeti la VG nchini Norway, Solskjaer alikiri kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ya msimu ujao ugani Old Trafford ni kumsajili Haaland na ni matarajio yake kwamba sogora huyo atakuwa hiari kuungana naye ikizingatiwa uhusiano waliokuwa nao kambini mwa Molde.

“Tuijivunia wakati murua wa takriban miezi 18 hivi kambini mwa Molde. Takriban miaka miwili. Kwa sasa anajivunia wakati maridhawa katika taaluma yake na atakuwa miongoni mwa wanasoka matata zaidi duniani,” akasema Solskjaer.

“Namfuatilia kwa karibu na dalili zote zinaashiria kwamba atapuuza baadhi ya ofa anazoelekezewa na kutua Man-United,” akaongeza kocha huyo.

Huenda ikawa rahisi zaidi kwa Haaland kushawishika kuagana na Dortmund iwapo waajiri wake hao wa sasa watakosa kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kufikia sasa, Dortmund wanashikilia nafasi ya sita jedwalini huku pengo la alama 16 likitamalaki kati yao na viongozi na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich wanaotiwa makali na mkufunzi Hansi Flick.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Leicester City watoka nyuma na kuendeleza masaibu ya...

Kenya yachagua timu imara ya Mbio za Nyika za Afrika