Kimataifa

Somalia yaambia balozi wa Ethiopia akanyage nje huku uhasama ukizidi kutokota

April 5th, 2024 1 min read

NA ABDULKADIR KHALIF

SOMALIA imefurusha balozi wa Ethiopia nchini humo huku uhasama ukiendelea kutokota kati ya nchi hizo mbili kutokana na madai ya Ethiopia kuingilia masuala yake ya ndani.

Hatua hiyo ilijiri Alhamisi baada ya mkutano wa baraza la mawaziri ulioongozwa na Waziri Mkuu Hamza Barre ambapo iliamuliwa kwa balozi Muktari Mohamed Ware afukuzwe ‘mara moja.’

Kulingana na taarifa kutoka afisi ya Hamza, Ethiopia imezidisha mwenendo wake wa kuingilia masuala ya Somalia.

Serikali ya Somalia ilionekana kukerwa na tangazo la eneo la Puntland, linalotaka kujitenga, kuwa limebuni ushirikiano mpya na Ethiopia.

Hii ni baada ya utawala wa eneo kujiondoa kutoka mfumo wa utawala wa majimbo wa Somalia na kutangaza kuwa itajitawala kama nchi huru.

Puntland ilikataa marekebisho yaliyofanyiwa sura nne za Katiba licha ya marekebisho hayo kuidhinishwa na bunge la Somalia, siku moja iliyotangulia.

Somalia na Ethiopia zimekuwa zikizozana kuhusu udhibiti wa eneo la Somaliland tangu Januari mwaka huu. Hii ni baada ya Somaliland kutia saini mkataba (MOU) unaoiruhusu Ethiopia kukodisha bandari fulani eneo hilo kwa matumizi ya kibiashara.

Hata hivyo, wakati huo, Somalia haikumfurusha balozi Ware na wanajeshi wa Ethiopia wamesalia Somalia wakishiriki mpango wa kudumisha amani chini ya mwavuli Kikosi cha Umoja wa Afrika (ATMIS).

Lakini baada ya Ethiopia kutia saini mkataba huo na Somaliland, Somalia iliondoa balozi wake jijini Addis Ababa.

Uhasama kati ya Ethiopia na Somalia umendelezwa zaidi na hatua ya Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Ethiopia kupokea ujumbe kutoka Puntland Jumatano.