Kimataifa

Somalia yamuita balozi wake wa Kenya mzozo ukitokota

November 30th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

NAIROBI, Kenya

SOMALIA imemfukuza balozi wa Kenya nchini humo huku mzozo mpya katika ya nchi hizi mbili ukitokota.

Mnamo Jumapili, serikali ya Somalia ilimuita balozi wake Kenya Mohamoud Ahmed Nur ‘Tarzan’ kurudi Mogadishu kwa mashauriano na ikamuagiza balozi wa Kenya Lucas Tumbo kuondoka.

Somalia inalaumu Kenya kwa kushinikiza viongozi wa jimbo la Jubaland kukataa makubaliano yanayohusu uchaguzi unaotarajiwa mwezi huu.

Kwenye mkataba huo uliotiwa saini Oktoba, pande zote zilikubaliana raia wa Somalia kuchagua wabunge moja kwa moja.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Somalia Mohammed Ali Nur, alilaumu Kenya kwa kusukuma kiongozi wa Jubaland Mohamed Ahmed Madobe kukataa mfumo huo wa uchaguzi.

“Somalia inasikitishwa na hatua ya serikali ya Kenya ya kuingilia masuala ya ndani na kisiasa ya serikali ya majimbo ya Jamhuri ya Somalia inayoweza kuwa kuzingiti kwa uthabiti, usalama na maendeleo ya eneo nzima,” Bw Nur alidai.

“Serikali ya Somalia imetambua kuwa serikali ya Kenya inamwekea presha Rais wa jimbo la Jubaland, Bw Ahmed Mohamed Islan Madobe kwa lengo la kuendeleza ajenda yake ya kisiasa na kiuchumi Somalia,” alidai bila kutoa ushahidi wowote.

Madai hayo yanajiri siku chache baada ya Somalia kufungua ubalozi wake Nairobi uliofungwa nchi hiyo ilipokubwa na ghasia nayo Kenya ikafungua upya jengo mpya la ofisi za ubalozi wake jijini Mogadishu iliyojenga kuanzia 2018.

Somalia ilimfuta waziri wa mashauri ya kigeni Ahmed Isse Awad, aliyefungua ubalozi wake Nairobi.

Hii ni mara ya pili ya Somalia na Kenya kuzozana mwaka huu.

Mnamo Februari 2020 Kenya ilimuita balozi wake kurudi Nairobi kwa mashauriano na kumuagiza Tarzan kuondoka Nairobi. Hii ilitokea Somalia ilipojaribu kuuza sehemu ya bahari yenye utajiri wa mafuta ambayo nchi hizi mbili zinazozania.

Mnamo Jumapili, katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya Macharia Kamau alisema kwamba hatua ya Somalia ya kumuita nyumbani balozi wake Kenya inasikitisha.