Habari Mseto

Somo la mazingira ya kiafya latiliwa mkazo MKU

July 30th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kutilia mkazo mazingira ya kiafya hasa katika masomo katika vyuo vikuu nchini, amesema waziri.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alisema ni muhimu kuzingatia masomo hayo katika vyuo vikuu ili kuboresha afya ya umma, hasa katika makazi.

Alisema bodi kuu ya kutazama maswala hayo imekuwa ikiendesha masomo hayo katika vyuo tofauti hapa nchini.

Mwenyekiti wa Baraza la Wahudumu wa Afya na Wataalamu wa Meno, Kenya Medical Practioners and Dental Council, Dkt Eva Njenga alisoma hotuba kwa niaba ya waziri Kariuki.

Dkt Njenga alisema Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kitaendelea kuwapa wanafunzi masomo kuhusu mazingira ya kiafya.

Alisema wataalamu katika sekta hiyo wanahitajika kwa wingi.

Dkt Eva Njenga (katikati) akiwa katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya. Picha/ Lawrence Ongaro

Kwenye hotuba yenyewe, waziri alisema mafunzo ya mazingira ya kiafya ni muhimu katika maisha ya mwanadamu kwa sababu yanatilia zingatio maswala ya uhifadhi wa chakula.

Dkt Njenga alisoma hotuba hiyo katika MKU wakati wa kutoa vyeti kwa wanafunzi waliofuzu kwa somo la mazingira ya kiafya.

Alisema wanafunzi hao waliofuzu wataangazia mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira, na utumizi wa sigara ambayo imetajwa kama hatari kwa sababu husababisha maradhi ya saratani.

Afisa kujisajili

Alisema serikali imepitisha sheria ya kwamba yeyote anayefuzu kuwa afisa wa afya ya umma ni sharti ajisajili rasmi na awe na leseni inayotambulika na bodi ya afisa mkuu wa afya ya umma, na kamati ya kiufundi katika idara hiyo.

Alifafanua kuwa kulingana na sheria nambari 12 ya mwaka wa 2013, ni sharti kuwe na udhibiti fulani wa kuendesha kazi hiyo.

“Leo ni siku kuu ya kuwapata maafisa waliofuzu rasmi katika somo hilo la Mazingira ya Afya kutoka Chuo hiki cha Mount Kenya na kwa hivyo wataonyesha weledi wao watakapokwenda katika mazingira ya umma kufanya kazi,” alisema Dkt Njenga alipowahutubia waliofuzu katika chuo hicho.

Alisema masomo hayo yanastahili kusambazwa hadi katika matawi mengine ya chuo hicho katika maeneo mengine.

Aidha, aliongeza kwamba serikali kuu itashirikiana na zile za kaunti ili kuhakikisha wafanyakazi wanaotumwa mashinani katika kaunti zingine wanaendesha mambo yao kwa njia ya uwazi bila kuingiliwa na yeyote.

Alisema serikali inaelewa masaibu yanayoshuhudiwa katika maeneo mengi ambapo itaweza kuingilia kati ili kuyatatua.

Naibu Chansela wa MKU Prof Stanely Waudo alisema chuo hicho kitafanya juhudi kuona ya kwamba kinawapa wanafunzi masomo ya kiwango bora ikiwemo ngazi za uzamili na uzamifu ili kuwapata wasomi wenye ujuzi kamili.

“Tungetaka kupata wataalamu zaidi wa kiwango cha juu ambao wataweza kujituma katika nchi za mbali kusambaza ujuzi wao huko. Hayo yatatimia tu iwapo tutakuwa na waliofuzu kamili katika kiwango cha juu cha masomo,” alisema Prof Waudo.