Michezo

Son afunga mabao manne na kuongoza Spurs kupepeta Saints 5-1

September 21st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Son Heung-Min alifunga jumla ya mabao manne katika ushindi wa 5-1 uliosajiliwa na Tottenham Hotspur dhidi ya Southampton uwanjani St Mary’s mnamo Septemba 20, 2020.

Mabao yote ya nyota huyo raia wa Korea Kusini yalichangiwa na nahodha Harry Kane aliyepachika wavuni goli la tano la Spurs kunako dakika ya 82.

Southampton walianza mchezo kwa matao ya juu na wakajipata kifua mbele kupitia kwa Danny Ings aliyefunga katika dakika ya 32. Ings aliwapa waajiri wake bao la pili kupitia penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.

Bao la kwanza la Son lilipatikana mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya kushirikiana tena na Alex McCarthy na kufunga goli la pili katika dakika ya 47.

Mabao mengine ya Son yalifumwa wavuni katika dakika za 64 na 73 kabla ya Erik Lamela kuchangia goli la tano la Spurs.

Mchuano huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa Southampton kupoteza katika mashindano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu. Kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Spurs, Southampton walikuwa wamepokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Crystal Palace katika mechi ya kwanza ya msimu huu ligini kabla ya Brentford kuwabandua kwenye raundi ya pili ya EFL Cup kwa mabao 2-0 mnamo Jumatano iliyopita.

Spurs walijitosa ugani wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi wao wa kwanza katika EPL msimu huu baada ya kulazwa 1-0 na Everton mnamo Septemba 13 kisha kutolewa jasho na Lokomotiv Plovdiv ya Bulgaria kwenye Europa League mnamo Septemba 17.

Kusuasua kwa Dele Alli katika mechi mbili za kwanza zilizosakatwa na Spurs muhula huu kulichangia kutemwa kwake katika kikosi cha kwanza dhidi ya Southampton na marejeo ya Gareth Bale huenda ziwe habari mbaya zaidi kwa Mwingereza huyo.

Ushirikiano kati ya Bale, Son na Kane unatazamiwa kuwa tishio kubwa zaidi kwa wapinzani wa Spurs katika kampeni za msimu huu nchini Uingereza na kwenye soka ya bara Ulaya.

Southampton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Burnley ugenini mnamo Septemba 26 huku Spurs wakiwaendea Leyton Orient katika raundi ya tatu ya League Cup mnamo Septemba 22, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO