Habari Mseto

Sonko aagiza wahalifu wasalimishe silaha haramu

November 12th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

MAGENGE ya wahalifu Kaunti ya Nairobi yameonywa vikali huku viongozi wakiapa kutwaa silaha haramu wanazotumia katika juhudi za kukomesha wimbi la mauaji na wizi jijini.

Haya yalijiri baada ya Gavana Mike Sonko kuwapatia wafuasi wa genge hatari la Gaza Boys linalohangaisha wakazi wa mtaa wa Kayole siku saba kusalimisha silaha zote haramu walizonazo na kuahidi kuwasamehe a watakaofanya hivyo.

Wafuasi wengi wa genge hilo wameuawa katika muda wa miaka miwili iliyopita lakini wakazi wa Kayole wanalalamika kwamba genge hilo limeundwa upya na limekuwa likiwahangaisha.

Bw Sonko alieleza kuwa watakaoitikia wito wake wa kusalimisha silaha watapatiwa nafasi za kazi lakini wale ambao watapuuza na kuendelea kuhangaisha wakazi wa Nairobi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Nilikuwa mwizi mkubwa zamani lakini uamuzi wangu wa kuacha kuhusika na uhalifu ulibadilisha maisha yangu hadi nilipo sasa. Nina uwezo wa kubadilisha maisha ya vijana hawa wahalifu iwapo watajisalimisha,” alisema Bw Sonko.

Alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki akiwa eneo la Matopeni alipoongoza harambee ya kumchangia Harrison Karanja almaarufu Papa, pesa za kulipa bili ya hospitali. Bw Karanja alipigwa risasi mara nne na watu walioshukiwa kuwa wafuasi wa genge la Gaza Boys mtaani Kayole mnamo Septemba.

Karanja amekuwa hospitalini tangu wakati huo na bili imefikia Sh5.1 milioni.

Bw Sonko alimtaka diwani wa eneo hilo, Bw Abdi Guyo kukutana na machifu, wafuasi wa genge hilo wanaojulikana na wazazi wao ili kuwashawishi waache uhalifu. Aliwataka vijana kulenga kujiajiri au kutafuta kazi badala ya kushiriki uhalifu.

Kwa upande wake Bw Guyo ambaye ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Nairobi aliwataka wakazi kutowakubali viongozi wanaounga na kufadhili makundi ya wahalifu.