Sonko aandamana na wakili wake hadi afisi za DCI

Sonko aandamana na wakili wake hadi afisi za DCI

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko Jumatatu alifika katika makao makuu ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuhojiwa na kufunguliwa mashtaka ya kudharau afisi ya Rais baada ya mahakama kuu kutupilia mbali kesi ya kuzima agizo afike mbele ya Naibu wa Inspekta Jenerali John Kariuki kujibu maswali kadha.

Punde tu baada ya Jaji James Makau kukataa ombi la Bw Sonko la kupiga breki agizo ajisalamishe katika afisi ya DCI kueleza masuala mbalimbali kutokana na matamshi yake, wakili Dkt John Khaminwa alisema, “ Nitaandamana na mlalamishi (sonko) hadi afisi za DCI.”

Akitoa uamuzi , Jaji Makau alisema hawezi kuzuia maafisa wa polisi wakitekeleza majukumu yao.

“Kazi ya polisi ni kupambana na uhalifu, kudumisha sheria na utangamano na kamwe hii mahakama haiwezi kuwazuia wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba,” alisema Jaji Makau.

Hata hivyo Jaji huyo aliratibisha kesi aliyowasilisha wakili wa Bw Sonko, Dkt John Khaminwa kuwa ya dharura.

Bw Sonko alikuwa amewashtaki Katibu Mkuu katika Afisi ya Rais anayehusika na usalama wa ndani Dkt Karanja Kibicho, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, Naibu wa Inspekta Jenerali John Kariuki, Inspekta Jenerali (IG) Hilary Mutyambai, Mwanasheria Mkuu, Chama cha Orange Democratic Movement na Mamlaka Huru ya Polisi (IPOA).

Bw Sonko alikuwa ameomba mahakama imzuie Bw Kariuki asimhoji kutokana na matamshi yake hivi majuzi kuhusu masuala nyeti ya uchaguzi mkuu wa 2017.

“Naomba hii mahakama isitishe agizo Bw Sonko afike mbele ya Bw Kariuki kuhojiwa kufuatia agizo la Dkt Kibicho kwamba alitoa matamshi ya kudunisha afisi kuu ya Rais,” Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Makau .

Dkt Khaminwa alisema kuwa Bw Sonko hapasi kuchukuliwa hatua kwa kusema atawaeleza Wakenya kilichojiri kuhusu matokeo ya kura za uchaguzi mkuu wa 2017.

Aliomba mahakama ipige teke agizo Bw Sonko afike mbele ya Bw Kariuki kushtakiwa kwa makosa ya kudunisha afisi kuu ya umma kinyume cha sheria nambari 132 cha sheria.

Shtaka la pili ni kuwa alichochea ghasia na vurugu. Akipinga Bw Sonko asifike katika afisi ya DCI Dkt Khaminwa alisema haki zake zitakandamishwa na uhuru wake wa kusema umekiukwa.

You can share this post!

Aibu wabunge wakilimana makonde mazishini

Rais awaongoza vigogo wa siasa kumwomboleza Nyachae