Habari Mseto

Sonko aapa kunasa matatu zinazoingi katikati ya jiji

August 13th, 2018 2 min read

Na COLLINS OMULO

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imeapa kuendelea kunasa magari yanayokiuka sheria inayopiga marufuku matatu kuingia katikati mwa jiji.

Kulingana na sheria zilizotolewa wiki iliyopita, ni magari mawili pekee ya kila chama cha ushirika (Sacco) yanaruhusiwa kuingia katikati mwa jiji.

Matatu hizo zinazoruhusiwa kuingia katikati mwa jiji zimepewa dakika tano pekee kushusha na kubeba abiria na kisha kuondoka.

Mkurugenzi wa Operesheni wa Kaunti ya Nairobi Peter Mbaya alisema tayari wamenasa matatu 30 ambazo zimekiuka agizo hilo tangu Jumatatu, wiki iliyopita.

“Agizo hilo halijafeli kama inavyodaiwa. Baadhi ya Sacco zinaonekana kukiuka sheria hizo na tutaendelea kunasa magari yanayokaidi. Kufikia Ijumaa, tulikuwa tumenasa matatu30,” akasema Bw Mbaya.

Bw Mbaya alisema matatu zinazohudumu katika maeneo ya Ronald Ngara ndizo zinaongoza katika ukiukaji wa sheria hiyo.

Alisema magari yanayomilikiwa na Sacco za 145, Kenya Mpya yamepuuza sheria hiyo huku akipongeza matatu za Saccco ya Ummoinner kwa kuitii kikamilifu.

“Tuna matumaini kuwa magari ya Sacco zote yatazingatia kikamilifu agizo hilo, la sivyo tutayakamata,” akasema.

Mkurugenzi huyo alisema kila gari ambalo limenaswa litatakiwa kulipiwa faini ya kati ya Sh15,000 na Sh30,000 kabla ya kuachiliwa.

“Magari hayo yanapokamatwa na kufikishwa katika eneo la kuegesha, mhusika sharti alipe faini ya Sh15,000. Gari linaposalia katika eneo hilo kwa siku mbili mwenyewe atatozwa faini ya Sh25,000 na zaidi ya siku mbili faini itakuwa Sh30,000,” akasema.

Sheria hiyo ya Kaunti ya Nairobi, hata hivyo, imepingwa vikali na Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) ambao walisema kuwa serikali ingefanya uchunguzi na kubaini njia mbadala za kupunguza msongamano badala ya kupiga marufuku matatu kufika katikati mwa jiji.

Chama hicho kilisema kuwa hakikushauriwa katika uamuzi wa kuzuia matatu kufika katikati mwa jiji huku kikisisitiza kuwa hatua hiyo itaathiri pakubwa biashara zao.

“Serikali ya kaunti inastahili kutuhusisha katika kufanya maamuzi muhimu yanayoathiri biashara zetu,” akasema mwenyekiti wa MWA Simon Kimutai.

Lakini hii si mara ya kwanza kwa serikali ya kaunti kutoa agizo sawa katika jaribio la kutaka kuzuia magari kufika katikati mwa jiji.

Mnamo Mei, mwaka huu serikali ya Gavana Mike Sonko ilitoa agizo sawa lililolenga kuzuia matatu 30,000 kufika katikati mwa jiji lakini likagonga mwamba.