Sonko adai kuna mtu alitaka kumdunga sindano ya sumu

Sonko adai kuna mtu alitaka kumdunga sindano ya sumu

Na RICHARD MUNGUTI

UFICHUZI wa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kwamba mtu aliingia kwenye seli anamozuiliwa katika kituo cha Polisi cha Gigiri akitaka kumdunga sindano ya sumu ulishtua kila mmoja.

Kupitia kwa mawakili Dkt John Khaminwa , Assa Nyakundi na Wilfred Nyamu, Sonko alisimulia akilia jinsi “ mtu alijaribu kumdhuru.” Licha ya kuwa anaugua presha, Sonko hakuitisha msaada wowote wa kimatibabu.

Sonko alisema anazuiliwa peke yake katika kituo cha polisi cha Gigiri kilichoko katibu na makao makuu ya shirika la umoja wa mataifa la mazingira (UNEP) na ubalozi wa Amerika.

“Usiku wa manane mtu aliyekuwa na sindano iliyokuwa na dawa isiyojulikana aliingia ndani ya seli anapozuiliwa Sonko na kujaribu kumdunga,” Dkt Khaminwa alimweleza hakimu mkuu Douglas Ogoti anayesikiza kesi ya ufisadi dhidi ya Sonko.

Dkt Khaminwa alisema Sonko alipiga duru hadi maafisa wa polisi waliokua kituoni wakakimbia kuona kilichokuwa kinaendelea.

“Nilipigiwa simu mwendo wa saa nane niende kituo cha polisi cha Gigiri kumwona Sonko kwa vile alikuwa anapiga duru,” Dkt Khaminwa alieleza Bw Ogoti akionyesha masikitiko na mshangao.

Pia Dkt Khaminwa alisema “ ni jambo la aibu kwa polisi kumwamuru Sonko alale sakafuni bila gondoro.”

Wakili huyo alisema hakurudi Gigiri kwa vile alikuwa ametoka mle mwendo wa saa tano usiku lakini alimpigia Bw Nyakundi afululize hadi kituoni.

Wakili Dkt John Khaminwa. Picha/RICHARD MUNGUTI

Bw Nyakundi alieleza mahakama kwamba alienda hadi Gigiri mwendo wa saa saba usiku.

“Niliruhusiwa kuingia kituoni lakini sikukubaliwa kumwona Sonko,” alisema Bw Nyakundi.

Wakili huyo alisema endapo nchi hii itachukua mkondo huo wa kuwatesa washukiwa bila shaka itakuwa kama Pakistan, Uganda, Angola n ahata Tanzania miongoni mwa mataifa mengine.

Bw Nyakundi alieleza mahakama alishangaa kunyimwa fursa ya kumwona Sonko ikitiliwa maanani “mshukiwa yuko huru kuwasiliana na kuonana na wakili wake wakati wowote katika masaa 24.”

Bw Nyamu alisema usalama wa Sonko wahitaji kuzingatiwa na kila mmoja kwa mujibu wa Kifungu nambari 3 cha katiba.

Mawakili hao walimsihi hakimu aamuru Sonko ahamishwe na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga pamoja na mahabusu wengine.

Kiongozi wa mashtaka Alex Akula alipinga ombi hilo akisema Sonko aliagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri na hakimu mkuu wa Kiambu Bi Stella Atamba na kwamba “ agizo hilo haliwezi kubatilishwa na hakimu mwenye cheo sawa naye(atambo).”

Akitoa uamuzi Bw Ogoti alimwamuru afisa msimamizi wa kituo hicho cha polisi cha Gigiri (OCS) amtunze Sonko.

Bw Ogoti alisema usalama na haki ya Sonko sio mambo ya kuchezewa. Hakimu huyo aliamuru OCS huyo awakubalie mawakili wake Sonko kumwona wakati wowote.

Pia aliamuru daktari wa kibinafsi wa Sonko aruhusiwe kumwona. Sonko anakabiliwa na kesi kadhaa katika mahakama ya Milimani, Kiambu na Kahawa.

Mahakimu wanaosikiza kesi dhidi ya Sonko , Bw Ogoti, Bi Atambo na hakimu mkuu mahakama ya Kahawa Bi Diana Mochache anayesikiza kesi ya ugaidi dhidi ya Sonko waliamuru azuiliwe katika kituo hicho cha polisi-Gigiri.

You can share this post!

Leteni hoja hiyo tupambane nayo, Tangatanga waambia Savula...

Taabani kwa kuuza vifaa feki vya kupima Ukimwi