Habari

Sonko afika kuhojiwa makao makuu ya EACC

November 5th, 2019 1 min read

Na MARY WAMBUI

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko amekuwa na kibarua Jumanne kujieleza mbele ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (EACC) kuhusu kinachodaiwa kuwa ni kujaribu kuficha mabaya yake ya zamani.

Amehojiwa na wapelelezi wa EACC kwa muda wa saa kadhaa katika Jumba la Integrity, Nairobi.

Inadaiwa Sonko alikosa kutoa kwa EACC habari muhimu kuhusiana na msururu wa kesi za uhalifu dhidi yake mahakamani katika kipindi ambacho alikuwa akitaka idhini kuwania ugavana wa kaunti ambayo pia ni jiji kuu.

EACC inamtaka Gavana huyo kujibu tuhuma hizo, lakini pia ikimtaka aandikishe taarifa.

Sonko aliwasili Integrity Centre saa tano na nusu ikiwa ni kuchelewa kwa muda wa saa moja na nusu tangu muda uliokuwa umewekwa.

Alitaka kuingia akiwa katika gari, lakini walinzi pale langoni wakasisitiza ni lazima ashuke kisha atembee kwa miguu.

Kwenye kizaazaa kilichojiri, wanahabari kadha wamejeruhiwa.

Baadaye Sonko ameonekana akiingia huku akiwa na baadhi ya watu wake wa karibu na mawakili kadha.

Awali wafuasi wake walilazimika kutoroka baada ya maafisa kukabiliana nao katika ofisi za EACC na vilevile Uhuru Park.

Endapo atakutwa na hatia, gavana huyu mwenye mbwembwe huenda akafungwa jela miaka mitano, au alipe faini ya Sh5 milioni; na hata pia anaweza kuajibishwa adhabu zote mbili.