Habari MsetoSiasa

Sonko aiga Rais, ateua msimamizi wa shughuli za wizara zote

July 23rd, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Sonko ameiga hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuteua waziri atakayesimamia shughuli za wizara zote za kaunti.

Mapema mwaka huu, Rais Kenyatta alimchagua Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kusimamia wizara zote za serikali kuu.

Bw Sonko sasa naye amemchagua Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi katika Kaunti, Bw Charles Kerich, kusimamia mawaziri wengine wote wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ina mawaziri kumi wanaosimamia sekta mbalimbali.

Sawa na jinsi Dkt Matiang’i anavyoonekana kuwa waziri mwaminifu zaidi kwa Rais Kenyatta, Bw Kerich ameibuka kuwa waziri ambaye Bw Sonko anaonekana kumwamini zaidi serikalini mwake tangu alipojiunga na baraza lake la mawaziri kusimamia Wizara ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano.

Bw Kerich huandamana na Bw Sonko katika shughuli nyingi rasmi na pia ndiye huachiwa jukumu la kuhutubia wanahabari kuhusu masuala mazito yanayohusu usimamizi wa serikali hiyo.

Kufikia sasa, Bw Kerich amewahi kushikilia wizara nne tofauti ikiwemo Afya na Ardhi.

Bw Sonko alisema aliamua kuchukua hatua hiyo ili kuboresha utoaji huduma na utekelezaji bora wa miradi yote na mipango katika kaunti nzima.

Kulingana naye, uteuzi huo umefuata sheria zinazohitaji mamlaka za kiserikali zitumiwe kwa manufaa ya wananchi.