Habari MsetoSiasa

Sonko aililia mahakama imruhusu asafiri Dubai

February 5th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA Mike Sonko Jumatano aliomba mahakama imruhusu ahudhurie mkutano wa viongozi wa kimataifa unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu ustawi wa miji, jijini Dubai katika Milki za Uarabuni (UAE).

Bw Sonko aliyewasilisha ombi hilo siku moja baada ya mahakama kuamuru akaunti zake tano zifunguliwe aliambia korti “ mkutano huo unahudhuriwa na viongozi wateule kutoka mataifa mbali mbali ya ulimwengu.”

Lakini Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alipinga Bw Sonko akiruhusiwa kuhudhuria mkutano huo akiuliza, “atahudhuria mkutano huo kama nani na hatekelezi majukumu yake ya ugavana.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Eva Kanyuiro alimkumbusha hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti kuwa “Sonko hana idhini ya kutekeleza majukumu yoyote ya afisi yake hadi kesi inayomkabili ya ufujaji wa zaidi ya Sh357m pesa za umma isikizwe na kuamuliwa,” alisema Bi Kanyuira.

Bi Kanyuira , aliyeomba hakimu akatae ombi hilo aliomba muda afisi ya DPP ichunguze barua iliyomwalika bw Sonko kuhudhuria mkutano huo wa kimataifa wa viongozi kuhusu ustawi wa miji na uimarishaji wa maisha ya wakazi wa mitaa ya mabanda.

Wakili wa Gavana Sonko George Kithi alipomtetea mteja wake. Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilielezwa na Bi Kanyuira kuwa , afisi ya DPP ilikabidhiwa barua hiyo juzi ilhali ilipokewa katika Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Septemba 23 2019.

Mahakama ilifahamishwa ni Wizara ya Mashauri ya Kigeni ambayo ingelimteua Gavana Sonko kuhudhuria mkutano huo ulioko mjini Abudhabu katika milki za mataifa ya UAE.

“Nahitaji muda kuthibitisha mwaliko huu pamoja na barua anayotegemea Sonko kuomba korti ibadili masharti ya dhamana,” Bi Kanyuira.

Alisema miongoni mwa masharti 10 aliyopewa Gavana Sonko ni kutosafiri ng’ambo bila idhini ya mahakama.

Pia aliagizwa awasilishe pasipoti zake mahakamani ziwekwe na naibu wa msajili wa idara ya mahakama.

“Ushahidi alioawasilisha Sonko kuthibitisha anasafiri ni pamoja na nauli ya ndege aliyojilipia mwenyewe na ada za hoteli alizojigharamia kati ya Feburuari 8-15 2020,” alisema Bi Kanyuira.

Mahakama ilielezwa Sonko anaenda starehe zake na wala sio mwaliko rasmi kama ilivyosemwa na wakili George Kithi.

“Ingelikuwa ziara rasmi iliyondaliwa na UN kupitia kwa barua iliyotiwa sahini na katibu muhusika Bw Maimuna Mohd Sharriff , ingelisemwa hivyo,” alisema Bi Kanyuira alisema akiomba mahakama ikatae ombi la Sonko.

Kiongozi wa Mashtaka Eva Kanyuira. Picha/ Richard Munguti

Akiwasilisha ombi hilo Bw Kithi alimsihi hakimu amruhusu mshtakiwa huyo kuhudhuria mkutano huo wa kimataifa kuhusu ustawi wa miji na ufanikishaji wa maisha ya uchochole ya wakazi wa mitaa ya mabanda.

“Gavana Sonko haendi kwa starehe zake mbali alipokea mwaliko wa UN kuhusu makazi na uboreshaji miji na kuinua maisha ya wakazi wa mitaa ya mabanda,” alisema Kithi.

Wakili huyo aliomba mahakama imruhusu Sonko kusafiri na kutoa hakikisho, “mimi mwenyewe nitazirudisha pasipoti mbili za gavana huyu alizoleta hapa kortini kujisimamia alipoachiliwa kwa dhamana.”

Bw Kithi aliomba mahakama imruhusu Sonko kuiwakilisha nchi ya Kenya katika dhifa hiyo ya siku sita UAE.

Bw Ogoti ataamua leo ikiwa atamruhusu Sonko kusafiri au la.