HabariSiasa

Sonko akaangwa Mlima Kenya kwa kudai kuna njama ya kuzima Ruto 2022

March 27th, 2018 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

VIONGOZI wa eneo la Mlima Kenya, wamemshtumu Gavana wa Nairobi Mike Sonko, kwa kudai kwamba wanasiasa wa eneo hilo wanapanga kuhujumu azma ya Naibu Rais William Ruto ya kutwaa urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Viongozi hao walimtaka Bw Sonko kuacha kuingilia siasa za eneo lao na kukoma kutoa vitisho.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alisema Bw Sonko hafai kuzungumzia siasa za eneo la Mlima Kenya na kumlaumu kwa kuzua migawanyiko katika chama cha Jubilee ilhali jiji limesakamwa na matatizo tele.

“Hata hakupatia Jubilee kura kutoka jamii yake. Kuna zaidi ya watu 200,000 ambao walimpigia kura Nairobi lakini hawakupigia kura Rais Uhuru Kenyatta.

Anafaa kutueleza atakavyohakikisha Ruto atapata kura hizo,” alisema Bw Gachagua ambaye amekuwa akimuunga mkono Bw Ruto.

Alisema eneo hilo litamuunga Bw Ruto kwenye uchaguzi wa 2022 na akakanusha kuwa viongozi wamekuwa wakiandaa mikutano usiku kwa lengo la kumhujumu Bw Ruto ili asishinde urais 2022 .

Naye Mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu alimlaumu Bw Sonko kwa kupanda mbegu za uwoga na kutisha wapigakura zaidi ya milioni tano wa eneo hilo.

“Matamshi ya Bw Sonko hayatamsaidia Bw Ruto. Amevuka mpaka kwa kutoa madai ya uogo kutuhusu. Hakuna mikutano ya usiku na hata hivyo, hakuna kinachozuia viongozi kukutana,” alisema Bw Wambugu.

Aliwataka wanasiasa wanaompigia debe Bw Ruto kuacha kutoa vitisho na kuheshimu uhuru wa kujieleza.

Alisema iwapo Bw Ruto anataka kuungwa mkono ni lazima aendelee kuungana na Rais Uhuru Kenyatta kutimiza malengo yake ya maendeleo.