Habari MsetoSiasa

Sababu ya Sonko kukimbizwa hospitalini

December 10th, 2019 1 min read

MARY WANGARI NA RICHARD MUNGUTI 

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko Jumanne amepokea matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Bw Sonko aliondolewa kutoka gereza kuu la Kamiti kupelekwa KNH kwa ushirikiano wa maafisa wa idara ya magereza, afisa mkuu wa polisi anayechunguza kesi ya ufisadi wa Sh381 dhidi ya gavana huyu na mawakili wake wakiongozwa na George Kithi.

Kufikia saa nane alasiri Bw Kithi na watu wa familia ya Sonko walikuwa wanashughulika alazwe KNH kulingana na agizo la hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Douglas Ogoti.

Jumatatu alasiri Ogoti aliamuru Sonko azuiliwe katika gereza lililo na kliniki ambaoi anaweza kupokea matibabu na akizindiwa “ apelekwe KNH” kwa matibabu maalum.

Kwa mujibu wa ripoti ya Dkt Esther Nekesa Wafula wa hospitali ya MP Shah aliyempima Sonko  Jumamosi alipendekeza afanyiwe ukaguzi zaidi ibainike ikiwa amevunjwa mbavu.

Sonko anahisi maumivu kifuani na kuumwa na mbavu.

Timu yake ya mawakili ikiongozwa na Cecil Miller, Jumanne walihoji mbele ya Hakimu Mkuu kuhusu Kukabiliana na Ufisadi Douglas Ogoti kwamba gavana huyo anayekabiliwa na wakati mgumu alikuwa mgonjwa na alihitaji huduma za matibabu baada ya kudhulumiwa na maafisa wa usalama waliomkamata Voi Ijumaa iliyopita,

“Kutokana na dharura ya matibabu ya mshukiwa (Mike Sonko), ingawa imepingwa, imeamrishwa kuwa kulazwa kwake hospitalini kutaidhinishwa na kituo cha matibabu gerezani mbele ya daktari wake ili asindikizwe katika hospitali nyingine yoyote kwa matibabu yake punde iwezekanavyo,” ulisema uamuzi wa hakimu Ogoti.

Kufuatia uamuzi huo, Sonko alitibiwa katika Gereza la kamiti jana jioni lakini uamuzi ukafanywa wa kumhamisha katika KNH.

Gavana huyo pamoja na wengine 12, walioshtakiwa mnamo Jumatatu dhidi ya hatia kadha za ufisadi, wanatazamiwa kuwasilishwa kortini tena Jumatano, Disemba 11, ambapo uamuzi utatolewa kuhusu maombi yao ya dhamana.