Habari Mseto

Sonko akubaliwa kuwafurusha wanabodaboda kutoka katikati ya jiji

March 26th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA wa bodaboda walipata pigo kuu Jumatatu baada ya Mahakama Kuu kutupilia kesi ya kupinga kumzuia Gavana Gedion Mike Sonko Mbuvi kuwatimua kati kati ya jiji.

Lakini Jaji Aburili aliwakashfu wanasiasa aliosema wanawatumia vibaya nyakati za siasa kisha wanawatupa baada ya uchaguzi.

Alisema wanasiasa wanawatumia wanabodaboda kama matambara katika siasa zao na baada ya kushinda viti wanawasahau ama kuwaacha na matumaini watawasaidia kuendelea na biashara zao katikati ya jiji.

Akikubalia kesi ya Sonko kuwa bodaboda ziondolewe katikati ya Nairobi, Jaji Aburili alimtaka  gavana huyo atumie weledi na makini anapowaondoa waendeshaji hao wa pikipiki.

“Waendeshao bodaboda hawapasi kutumiwa kama matambara yanayotupwa baada ya kutumiwa,” alisema Jaji Aburili.

Mahakama ilisema kulikuwa na kesi sawa na hiyo 2016 ambayo ilitupiliwa mbali.