Habari Mseto

Sonko aajiri upya mawaziri aliotimua

April 3rd, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Bw Mike Sonko amewarudisha kazini mawaziri wawili wa zamani baada ya wengine aliowateua kushindwa kuidhinishwa.

Aliyekuwa Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Bw Hitan Majevdia ambaye alikuwa amesimamishwa kazi Agosti mwaka uliopita, na aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi, Bi Vesca Kangogo aliyesimamishwa kazi Septemba mwaka uliopita, walirudishwa kazini Jumatatu.

Wawili hao watahudumu badala ya Bi Sonia Birdi ambaye licha ya kuteuliwa na Bw Sonko, alikataliwa na Bunge la Kaunti wiki mbili zilizopita, na Dkt Stella Bosire ambaye hakijitokeza kuhojiwa.

haya yalitangazwa rasmi Jumatatu jioni wakati mawaziri wengine watatu waliapishwa na gavana.

Watatu hao ni waliokuwa maafisa wakuu wa kaunti Winfred Kathagu na Lucia Mulwa ambao sasa watakuwa mawaziri, na aliyekuwa Kaimu Wakili wa KAunti, Bi Pauline Kahiga Waititu.

Bw Majvedia atakuwa Waziri wa Barabara, Uchukuzi na Miundomsingi huku Bi Kangogo akisimamia Wizara ya Mazingira naye Bi Kahiga akiwa katika Wizara ya Ugatuzi na Usimamizi wa Huduma za Umma.