Habari MsetoSiasa

Sonko alia kuhangaishwa na maafisa wa Ikulu

June 6th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko ameibua madai kwamba kuna maafisa katika Ikulu ya Rais wanaojitahidi kuvuruga utawala wake.

Alitoa madai hayo wakati ambapo anaendelea kukashifiwa vikali kwa kufichua mawasiliano ya siri anayodai yalikuwa kati yake na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris.

Gavana huyo amekuwa akianika peupe mawasiliano hayo kufuatia majibizano yaliyotokea kati yao wakati wa sherehe za Madaraka, akijitetea kwamba ni njia yake ya kujiondolea lawama kutokana na yale yaliyosemwa na Bi Passaris.

Usiku wa kuamkia jana, Bw Sonko alidai alikuwa na uhusiano mwema na Bi Passaris kwa muda mrefu na hakuamini jinsi mwakilishi huyo wa wanawake alivyomshambulia kwa maneno sikukuu ya Madaraka, akisema anaamini alikuwa ametumwa na maafisa wa Ikulu.

Kulingana naye, matatizo yake yalianza wakati wa ibada iliyofanywa kabla ya Leba Dei katika Kanisa la ACK la St Stephens lililo Jogoo Road, Nairobi, wakati alipokashifu maafisa anaodai ni wafadhili wa kikundi cha ‘Kieleweke’ kwa kujihusisha na ufisadi.

Kieleweke ni kikundi cha wanasiasa wanaopinga misimamo ya Naibu Rais, Dkt William Ruto na wandani wake.

“Mimi si mwanachama wa ‘kieleweke’ wala ‘tangatanga’. Hapo ndipo watu hao wamepotoka. Wanataka kuwa na mgombeaji wao wa ugavana mwaka wa 2022 ndiposa wananihangaisha,” akasema gavana huyo.

Aliendelea kudai bila thibitisho kwamba amewahi kushambuliwa nyumbani kwake, na akahusisha mahasimu hao wake na shambulio lililofanywa kwa binti yake, Bi Saumu Mbuvi alipokuwa akivinjari na Seneta wa Lamu, Bw Anwar Loitiptip usiku wa kuamkia Jumapili.

Mbali na haya, alidai pia uamuzi wa serikali kuu kwamba magavana wasifunguliwe njia wanapokuwa barabarani ulishawishiwa na maafisa hao wa Ikulu.

Hii si mara ya kwanza Bw Sonko kulalamika kuhusu maafisa wa Ikulu anaodai wanahujumu utawala wake.

Mwaka uliopita wakati wa hafla ya upandaji miti katika Shule ya Moi Forces Academy jijini Nairobi, gavana huyo alionyesha hasira wakati Waziri wa Mazingira, Bw Keriako Tobiko alipomwita Naibu Rais, Dkt William Ruto kuhutubu kabla gavana huyo kuzungumza.

Gavana Sonko amekuwa akizua ubishi wa kila aina tangu alipochaguliwa.