Habari Mseto

Sonko alilia mahakama itupe kesi dhidi yake

February 19th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA Mike Sonko Jumatano aliomba mahakama ifutilie mbali kesi tatu za ufisadi zinazomkabili akidai tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) ilikiuka sheria katika kupokea ushahidi iliyotegemea kumfungulia mashtaka kutoka kwa benki tano.

Kupitia kwa mawakili Cecil Miller na George Kithi, Bw Sonk alimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti atupilie mbali kesi tatu za ufisadi zinazomkabili.

Akiwasilisha ombi hilo , Bw Miller alimweleza hakimu kuwa EACC ilikaidi sheria ilipoomba wakuu wa Benki za Equity , Co-operative, Diamond Trust Bank (DTB), Kenya Commercial (KCB) na First Community waipe taarifa muhimu kuhusu akaunti za Sonko.

Bw Miller alisema vifungu nambari 27 (3) na 28 za sheria za kupambana na ufisadi na Kifungu nambari 50 (4) cha Katiba zinatoa mwelekeo wa kupokea ushahidi wa benki.

“Kifungu nambari 27 (3) cha sheria za kupambana na ufisadi kimeamuru wachunguzi wa ufisadi kutoa arifa kwa mshukiwa kabla ya kuchunguza akaunti zake za benki,” alisema Bw Miller.

Wakili huyo alisema kifungu nambari 28 kinaruhusu ushahidi wa miezi sita tu kutwaliwa kutoka kwa benki.

Mahakama ilifahamishwa EACC iliomba benki hizo tano kutoa ushahidi wa akaunti za Sonko kati ya Januari 2012 na Desemba 2019.

“EACC ilikaidi sheria kwa kuitisha ushahidi wa miaka saba badala ya miezi sita,” alisema Miller.

Mahakama ilifahamishwa Sonko hakupewa arifa na EACC kwamba akaunti zake zinachunguzwa ndipo awape nakala za ushahidi uliotakikana.

“ Sheria inaamuru ushahidi utolewe wa kipindi cha miezi sita. EACC iliitisha benki ushahhidi wa miaka saba,” alisema Bw Miller.

Wakili huyo aliomba mahakama ifutilie mbali kesi tatu za ufisadi alizoshtakiwa Sonko kwa “ vile ushahidi ulipatikana kinyume cha sheria.”

Mahakama ilifahamishwa kuwa Kifungu nambari 50 (4) cha katiba kinasema ushahidi uliopatikana kinyume cha sheria haupasi kukubaliwa mahakamani.

EACC ilipinga ombi hilo ikisema kuwa Sonko alijulishwa kuhusu ushahidi huo alipohojiwa Septemba 3 2019.

Tume hiyo iliomba mahakama iruhusu kesi dhidi ya Sonko ziendelee ikisema Sonko alifahamihswa kila kitu alipoagizwa afike kuandikisha taarifa katika afisi za EACC.

“Mahakama ya Juu ilifutilia mbali sheria hiyo ya kutaka mshukiwa apewe arifa kabla ya kuchunguzwa kwa akaunti zake za benki,” EACC ilieleza mahakama Sonko alikuwa anajua akaunti zake zina chunguzwa.

EACC ilimweleza kuwa Sonko ameshtakiwa kutokana na pesa zilizowekwa katika akaunti za benki ya Equity na kwamba uchunguzi unaendelea kufanywa katika benki zile nyingine nne.

Bw Ogoti atatoa uamuzi wake Feburuari 26, 2020.

Alipokuwa kortini Jumanne , Sonko , hakimu alishutumu afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na EACC kwa kutowapa ushahidi Gavana Mike Sonko na washukiwa wengine.

“Hii mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi za ufisadi na huku ni afisi za DPP na EACC zinazokawia kuwasilisha ushahidi,” alisema Bw Ogoti.

Hakimu huyo alisema atasimama kidete kuhakikisha sheria imefuatwa na afisi za DPP na EACC ndipo haki itekelezwe katika kesi za ufisadi.

Bw Ogoti alisema hayo alipoelezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Nanjala kwamba “nakala za mashahidi hazijakabidhiwa washtakiwa kufuatia agizo la mahakama kuu kwamba baadhi ya mashahidi wawekwe chini ya uangalizi wa kitengo cha kulinda mashahidi maalum (WPA).”

Hakimu alielezwa kufuatia agizo hilo la Mahakama kuu afisi ya DPP itaondoa ushahidi wa mashahidi watakaowekwa chini ya uangalizi wa WPA katika orodha na kuwapa majina bandia kabla ya kesi kusikizwa.

Mahakama ilielezwa nakala za ushahidi zimepewa washtakiwa isipokuwa washukiwa wawili Wambua Ndaka na Patrick Mwangangi.

Akihojiwa na Bw Ogoti afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Idris Garane alisema hakuelewa barabara agizo la Janauri 27 2020 kwamba awape Bw Sonko na washukiwa wengine nakala za ushahidi katika muda wa siku 14.