Habari

Sonko alivyojikaranga

December 8th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

SIKU moja baada ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko kutiwa mbaroni, polisi wamesema kwamba watamfungulia mashtaka zaidi ya uhalifu kufuatia purukushani zilizozuka akikamatwa.

Idara ya Polisi ilisema kwamba itamfungulia mashtaka kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi na kuzuia kutiwa mbaroni mjini Voi Ijumaa.

Kwenye taarifa, polisi walisema kwamba Bw Sonko alimpiga afisa wa cheo cha juu aliyesimamia operesheni ya kumkamata na kisha akaharibu kamera ya wanahabari.

Kesho, Bw Sonko atawasilishwa mahakamani Nairobi kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya Sh357 milioni, mali ya serikali ya Kaunti ya Nairobi, kupitia kwa utoaji wa zabuni kinyume cha sheria.

Jumamosi, Msemaji wa Polisi Charles Owino alisema Bw Sonko atafunguliwa mashtaka mengine ya kushambulia afisa wa polisi, kuwatusi maafisa wa polisi na kujaribu kukataa kutiwa mbaroni.

Hayo yalijiri Bw Sonko akilia kwamba maafisa waliomkamata walimtesa na kumjeruhi sehemu nyeti.

Wakili Harrison Kinyanjui alisema Bw Sonko anahitaji kupewa matibabu kwa dharura. Alisema Bw Sonko atahitajika kutumia mikongojo kutembea kufuatia mateso aliyopata mikononi mwa polisi.

Alisema afisa wa polisi ambaye alinaswa kwenye kamera za wanahabari akimpiga na kumburura Sonko kwa nguvu anafaa kukamatwa na kushtakiwa.

“Polisi watundu waliotendea unyama Gavana Sonko kule Voi wanafaa kukamatwa kwa kukiuka sheria na maadili ya kazi yao,” Bw Kinyajui alisema kupitia kwa taarifa iliyotolewa na afisi ya mawasiliano ya Sonko.

Hata hivyo, kulingana na Bw Owino, Gavana Sonko ataongezewa mashtaka zaidi sio tu kwa kushambulia maafisa wa polisi bali pia kuwazuia “kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria”.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi itamshtaki Gavana Sonko kwa sababu wakati alipokuwa akikamatwa alimshambulia afisa wa cheo cha juu ambaye alikuwa akiongoza shughuli hiyo na kuharibu vyombo vya wanahabari,” akasema.

Wakati huo huo , Bw Owino ameonya watu ambao inadaiwa wanapanga kufanya maandamano jijini Nairobi kupinga kukamatwa kwa Sonko akiwataka kufanya hivyo kulingana na sheria za Kenya.

“Tungependa kujulisha umma kwamba tumepokea ripoti kuwa kundi fulani la watu linapanga kufanya maandamano na kuvuruga utulivu maeneo kadhaa jijini Nairobi.”

“Kwa hivyo, umma unajulishwa kwamba watu ambao wanapanga kukongama kwa lengo la kufanya maandamano wanahitaji kuzingatia sheria,” Bw Owino alisema kwenye taarifa hiyo. Bw Sonko alikamatwa Ijumaa mjini Voi kufuatia amri iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashataka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

“Nimeamuru kukamatwa mara moja na kushtakiwa kwa Mike Sonko na maafisa wengine wa serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa makosa mbalimbali ikiwamo kupokea pesa kinyume cha sheria, kuchukua mali ya umma kinyume cha sheria, ulanguzi wa fedha na aina nyingine za uhalifu wa kiuchumi,” akasema Bw Haji.

Polisi walidai kuwa alinuia kutorokea Tanzania kuepuka kukamatwa lakini wakatibua mipango yake. Bw Sonko amekanusha madai hayo akisema alikuwa akienda Mombasa kuhudhuria mkutano wa wafanyakazi wa serikali yake.

Aidha, alikanusha kwamba alikuwa amefunga simu zake. Hata hivyo, polisi wanasisitiza kuwa alijaribu kupiga polisi na kukataa kutiwa mbaroni na watamfungulia mashtaka kulingana na sheria husika.