Bambika

Sonko ampeleka Kimani Mbugua kwa ‘rehab’ jijini Mombasa

June 8th, 2024 1 min read

NA MARGARET MAINA

ALIYEKUWA mwanahabari wa runinga ya Citizen, Kimani Mbugua, amepelekwa kwa ndege hadi jijini Mombasa ili kuingia rasmi kwa kituo cha urekebishaji almaarufu ‘rehab’ ambacho huwasaidia waraibu na wenye changamoto mbalimbali.

Gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko kupitia kurasa za akaunti zake za Facebook na X alisema Ijumaa kwamba ahadi aliyokuwa ameweka awali sasa ilikuwa inatekelezwa.

Awali, alikuwa ameahidi kumpeleka Mbugua kwenye kituo cha ‘rehab’ ambapo pia malkia wa masumbwi Conjestina Achieng yupo.

“Jana (Alhamisi), tulifanikiwa kumpeleka aliyekuwa mwanahabari wa Citizen TV Kimani Mbugua kwenye kituo cha urekebishaji na uwezeshaji kilichoko Mombasa kwa matibabu zaidi kama nilivyokuwa nimeahidi awali wakati wa mahojiano na Oga Obinna. Naomba tumuombee. Nina uhakika atakuwa sawa,” akaandika Bw Sonko.

Mnamo Mei 2024, Bw Sonko alimtembelea Mbugua katika Hospitali ya Mathari ambapo alikuwa akifanyiwa uchunguzi wa kiafya.

“Niliwatembelea Hospitali ya Mathari pamoja na Oga Obinna na familia ya Kimani Mbugua ili kuangalia wanavyoendelea (Kimani na Eunice Omollo). Tulipokelewa kwa upendo na madaktari wanaowahudumia, ambao walituambia kuhusu hali zao. Hata hivyo, Bi Omollo alikuwa anapokea matibabu kwenye wodi ya wanawake wakati wa ziara yetu, kwa hivyo nilifanikiwa tu kuwasiliana na Kimani (Mbugua),” akasema.

Alifichua kuwa alikuwa na wakati mzuri na Mbugua, wakikumbuka mahojiano ya zamani na kufanya mazungumzo ya kina kuhusu hali ya sasa ya mwanahabari huyo.

Mbugua amekuwa akisumbuliwa na hali ya matatizo ya afya ya akili inayofahamika kama bipolar disorder.

Kulingana na Bw Sonko, kumhamisha kutoka Mathari hadi Mombasa ni mabadiliko ya mazingira yanayoweza kusaidia katika mchakato wake wa kupona.

“Kimani Mbugua tayari alishatoa mengi kwa ulimwengu kupitia kazi yake na ni wakati wetu sasa wa kumrejeshea matumaini, upendo, na huduma,” akasema.

Mbugua alionekana akishuka kutoka kwa ndege na baba yake.

Mzazi huyo wake alielezea matumaini kwamba mwanawe atakuwa sawa.

[email protected]