Michezo

Sonko amsafirisha Conjestina hadi Nairobi kwa matibabu

November 2nd, 2018 1 min read

AYUMBA AYODI na PETER MBURU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amemnusuru mwanabondia wa kike ambaye aliletea Kenya sifa Conjestina Achieng’, baada ya maradhi ambayo amekuwa nayo ya akili kumzidia.

Gavana huyo aliahidi kuhakikisha kuwa Conjestina, ambaye ana miaka 41 ametibiwa kikamilifu kutokana na ugonjwa alio nao wa akili, baada ya kumsafirisha kutoka nyumbani kwao eneo la Gem, kaunti ya Siaya hadi Jijini Nairobi.

Msemaji wa gavana huyo Elikana Joseph alisema Conjestina atapokea matibabu katika kituo cha Eden Home Rehabilitation Centre.

Hii ilikuwa baada ya video kusambaa mitandaoni ikimwonyesha Conjestina akifanya mchezo na watu huku akipewa pesa, katika mandhari ambayo yaliibua hisia za huruma, haswa ikizingatiwa kuwa amewahi kuwa shujaa aliyeletea Kenya sifa kemkem alipokuwa mwanabondia takriban mwongo mmoja uliopita.

“Amefika Nairobi vizuri, mwanabondia huyo atapelekwa hospitali ya Nairobi West kufanyiwa uchunguzi kwanza kisha madaktari wataamua ambapo atalazwa kwa matibabu ya polepole. Karibu tena Conje,” Bw Sonko akasema kupitia akaunti yake ya Facebook jana.