Habari MsetoSiasa

Sonko amtimua waziri kwa kusafiri bila ruhusa yake

June 7th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amemtimua Waziri wa Ugatuzi wa kaunti, Bi Vesca Kangogo (pichani kushoto) kwa kusafiri ng’ambo bila ruhusa yake.

Hatua hii ilichukuliwa baada ya waziri huyo kusafiri kuelekea Amerika mnamo Ijumaa iliyopita licha ya kuwa Gavana alikuwa amemwambia asiende ziara hiyo.

Kwenye barua iliyoandikwa na Katibu wa Kaunti Peter Kariuki, Bi Kangogo ameamrishwa kwenda likizo ya lazima hadi atakapotoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kwa nini alisafiri bila ruhusa.

“Afisi hii imefahamishwa kuwa ulisafiri kwenda Amerika mnamo Juni 1, 2018, baada ya kuagizwa na gavana usisafiri.

Uamuzi wako kukiuka maagizo ya mwajiri wako ni sawa na ukaidi kwa hivyo, umemarishwa kung’atuka afisini,” sehemu ya barua hiyo ikasema.

Waziri huyo wa ugatuzi na usimamizi wa utumishi wa umma katika Kaunti amepewa siku saba kuwasilisha majibu yake. Siku hizo zitakamilika Jumanne ijayo.

Bi Kangogo alihudumu katika idara ya fedha wakati Bw Sonko alipoingia mamlakani baada ya kuhudumu kama naibu mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi wa Umma katika Kaunti wakati wa uongozi wa aliyekuwa gavana Dkt Evans Kidero.

Alihamishwa hadi katika idara ya ugatuzi wakati Bw Sonko alipofanya mageuzi katika baraza lake la mawaziri Februari.

Hii ni mara ya pili kwa Gavana kusimamisha kazi waziri kwa muda baada ya aliyekuwa waziri wa fedha na mipango ya kiuchumi kusimamishwa kazi kwa muda kisha baadaye akafutwa kazi kwa madai kuwa alikuwa akishirikiana na “maadui wa gavana”.

Hata hivyo, Bi Kangogo alisema hajapokea barua ya kumtimua akiahidi kujibu maswali kuihusu punde atakapoipokea.