HabariSiasa

Sonko anavyokwepa kukamatwa na DCI

September 19th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

MASAIBU yanayomkumba Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kuhusu kashfa za ufisadi yamkini yamemchochea kugeuza mienendo yake kwa namna ya kushangaza huku ikiaminika anajitahidi kuepuka kukamatwa ghafla na majasusi.

Gavana huyo ambaye ni maarufu kwa kujitokeza hadharani na kuzungumza kwa ujasiri mkuu, alishindwa hata kuhudhuria makumbusho ya miaka minne tangu kufariki kwa babake, wiki mbili zilizopita.

Duru zimefichua kuwa mnamo Septemba 6, Bw Sonko hakuwepo nyumbani kwake Mua Hills, Kaunti ya Machakos ambako makumbusho hayo yalikuwa yanafanywa.

Imebainika alielezwa na wandani wake kwamba makachero wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) walikuwa wakisubiri kumnasa.

“Alikuwa akielekea Mua lakini alipofika katika makutano ya barabara inayoelekea Chuo Kikuu cha Daystar, Athi River, aliambiwa kuhusu maafisa hao. Ilibidi ageuze gari lake akarudi Nairobi,” duru zilisema.

Alipowasili Nairobi, alienda moja kwa moja hadi katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege (JKIA) ambapo aliabiri ndege na kwenda Mombasa. Rais Uhuru Kenyatta alikuwa anafanya ziara Mombasa wakati huo.

Ikizingatiwa kwamba huwa hafichi jinsi alivyomthamini babake, tukio hilo lilionyesha namna gavana huyo amegeuka kuwa ndege anayewindwa na hivyo kukosa amani.

Taifa Leo imebainisha amezidisha tabia yake ya kubadili sehemu anazofanyia kazi tangu alipohojiwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) mnamo Septemba 3, huku Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) pia ikimwandama.

Vile vile, ameamua kuishi maisha ya kichini chini na kupunguza msafara wake mkubwa wa magari ili anapopita, isiwe rahisi kung’amua ni yeye yuko safarini.

EACC inamchunguza kuhusu utoaji zabuni ya Sh357 milioni kwa njia zinazodaiwa kukiuka sheria. Zabuni hiyo ilikuwa ya uzoaji taka jijini na ilipeanwa kwa kampuni 13.

Kwa upande mwingine, KRA inachunguza serikali yake kwa madai ya kukosa kuwasilisha Sh4.5 bilioni za ushuru, ikiwemo uliokatwa kutoka kwa wanakandarasi, na ushuru wa faida ambazo kaunti hupata.

Kutokana na haya yote, gavana huyo tayari amekiri hadharani kwamba atahitajika kuchagua naibu wake haraka iwezekanavyo ili kusiwe na pengo katika usimamizi wa kaunti endapo atashtakiwa.

Lakini kuna changamoto kwa kuwa mojawapo ya sababu zake kutochagua naibu tangu Bw Polycarp Igathe alipojiuzulu Januari mwaka uliopita ni kwamba, kuna watu wenye ushawishi katika Ikulu wanaomhangaisha wakitaka achague “mtu wao” kuwa naibu wake.

Endapo atashtakiwa, inahofiwa kutakuwa na pengo kubwa kwa kuwa hata Spika Beatrice Elachi anayetarajiwa kikatiba kuendesha kaunti iwapo hakuna naibu gavana, angali anakumbwa na misukosuko kutoka kwa madiwani waliomfurusha.

Ingawa wandani wake wanasema angependa zaidi kumchagua Mbunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA), Bw Simon Mbugua au Waziri wa Fedha katika Kaunti, Bw Charles Kerich kuwa naibu wake, angali anaandamwa na mapendekezo kutoka kwa watu wenye ushawishi serikalini.

Duru zetu zilisema alipokuwa Mombasa, alifanikiwa kuzungumza na Rais Kenyatta lakini haijulikani walijadiliana kuhusu jambo lipi.

Huku akiendeleza maisha hayo mapya, maafisa wa EACC na DCI huwa wanaonekana wakizurura katika makao makuu ya kaunti huku baadhi ya maafisa wakuu katika serikali hiyo wakiendelea kuhojiwa na KRA kuhusu suala la ukwepaji kulipa ushuru.