Habari

Sonko apata afueni mahakama ya Voi kufunga faili ya kesi dhidi yake

January 22nd, 2020 2 min read

LUCY MKANYIKA na MARY WANGARI

NI afueni kwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko baada ya mahakama ya Voi kufunga faili ya kesi ambayo mlalamishi – mkuu wa polisi Pwani – aliomba iondolewe.

Hii ina maana kwamba kesi ambayo Sonko alituhumiwa kutekeleza uvamizi na hivyo kumdhalilisha afisa imeondolewa.

Hakimu Mkuu Mkazi Frederick Nyakundi akitoa hukumu yake Jumatano asubuhi amesema kuna sababu za kutosha kulikubali ombi la mkuu wa polisi Pwani Rashid Yakub kuiondoa kesi hiyo.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) iliomba kusitisha mashtaka ya uvamizi aliyokabiliwa nayo gavana huyo.

Jumanne, upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba mlalamishi amehiari kuachana na kesi hiyo.

Wakili anayeongoza upande wa Sonko – mshtakiwa – Bw Cecil Miller alikuwa amekaribisha hatua hiyo.

Hatua hiyo ilikuwa afueni kuu kwa gavana huyo anayekabiliwa na mashtaka ya kufuja fedha za umma za Sh357 milioni yaliyomfanya kuzuiliwa kuingia afisini mwake.

Kufuatia uamuzi huo, Bw Sonko alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Facebook ambapo alichapisha video aliyonukuu “Mambo ya Mungu ni Mengi.”

Katika video hiyo ya kuibua hisia, bosi huyo wa kaunti alionekana kujitahidi kuzuia machozi ya furaha kumtiririka huku akionekana kufuta machozi alipoungana na wafuasi wake nje ya korti, kufanya ombi la shukran kwa Mungu.

Wafuasi wake pia hawakuachwa nyuma maadamu walifurika mitandaoni kwa jumbe za kumtia moyo huku wakimshukuru Mungu pamoja na gavana huyo.

“Tangu uanze maombi mambo yanaaenda vyema. Yote yakiisha usiache kuomba, Mweke Mola mbele na sisi wakaiz wa Nairobi,” alishauri Josia Deck.

“Mungu ni mwaminifu daima. Ndugu yangu Sonko nasimama nawe katika maombi. Mungu anaujua moyo wako na ndiposa utatoka ukiwa imara katika majaribu haya. Mwenyezi Mungu akuongoze,” alisema Shadrack Nyamai.

Baadhi ya wanamitandao walihoji kwamba moyo wa ukarimu na vitendo vya utu vya gavana huyo vilikuwa vimezaa matunda na ndiposa Mungu alikuwa amemnusuru.

“Walalahoi ambao wewe husaidia kila mara huwa wanakuombea. Mungu amekubariki kwa matendo yako mema. Usichoke kutenda mema,” akasema Levin Kidali kupitia maandishi aliyochapisha.

“Kwa sababu ya vitendo vyako vya kibinadamu, neema ya Mungu inafanya kazi mheshimiwa, Kibali kisichokuwa na kipimo. Hata kesi zilizosalia zitaisha kimiujiza,” alisema Rogers Maloi.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii hawakuridhishwa na hatua hiyo huku wakisisitiza kwamba afisa aliyeshambuliwa na gavana huyo pia alihitaji haki.

Walimtaka Sonko kumwomba radhi afisa huyo.

“Kama mnadai ni maombi yamefanya kazi na je, yule askari Sonko alipiga teke kwa hiyo video na kumwita shoga? Kwani yeye hana Mungu ama Mungu ana mapendeleo? Acheni kubebwa ufala na PR eti maombi. Hapa ni pesa imeongea,” alifoka Reuben Wafula.

“Ushuhuda mkuu unao ikiwa utamwomba msamaha afisa huyo…,” alishauri Sam Leen.

Wengine wamemshauri gavana huyo kumkumbuka mwananchi wa kawaida pindi atakaporejelea majukumu yake ikiwa ataondolewa lawamani.

“Si umesikia maisha huku nje ni magumu. Ukirudi ofisini utukumbuke sisi wafuasi wako,” akaandika mtumiaji mitandao anayejiita Anto Wambua.