Habari MsetoSiasa

Sonko apumua madiwani kusema hawatamng’atua

January 9th, 2020 1 min read

NA COLLINS OMULO

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amesema kwamba madiwani wa Bunge hilo la Kaunti hawatawasilisha mswada wowote wa kumng’atua Gavana Mike Sonko madarakani leo.

Hii ni licha ya kwamba bunge hilo limebuni kamati ya kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida katika serikali ya kaunti hata baada ya Gavana Sonko kuzuiwa kuingia afisini na mahakama mwezi uliopita.

Bi Elachi alisema kwamba kile ambacho kitajadiliwa kwenye mkutano huo wa leo ni namna ya kupambana kudorora kwa utoaji wa huduma katika kaunti na si jambo jingine ambao linahusu kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Bw Sonko.

“Kuna utaratibu wa kufuata ili kumwondoa gavana madarakani na hilo halitakuwa miongoni mwa hoja zitakazojadiliwa kwenye mkutano wetu. Tulichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali kwamba tutajadiliana kuhusu jinsi hali ilivyo katika kaunti na hatuwezi kuzua au kuleta suala jingine,” akasema Bi Elachi.

Alikuwa akisoma taarifa za madiwani wote 122 ambao waliandaa mkutano usio rasmi maarufu kama Kamukunji kujadilia masuala yanayoathiri maendeleo.

Bi Elachi aliongeza kwamba madiwani wanatambua kuwa kuna uongozi unaotambuliwa katika afisi za kaunti hata baada ya kushtakiwa kwa Bw Sonko.