Habari

Sonko asema yuko tayari kujiuzulu ili achunguzwe

September 6th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ametangaza kuwa ataondoka afisini – kwa muda – ikiwa atapatikana na hatia katika uchunguzi unaoendelea kuhusu sakata ya zabuni ya uzoaji taka katika Kaunti ya Nairobi.

Alisema hayo Alhamisi jioni alipowahutubia wanahabari baada ya kuhojiwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuri Nchini (KRA) kuhusiana na tuhuma nyingi ya kutowasilisha ushuru wa kima cha Sh4.5 bilioni tangu alipoingia mamlakani 2017.

Kuhusiana na sakata ya utoaji zabuni ya uzoaji taka, Bw Sonko anatuhumiwa kupokea mlungula kutoka kwa baadhi ya kampuni ambazo zimepewa zabuni hiyo tangu aingie mamlakani.

Inadaiwa kuwa baadhi ya kampuni zote 13 zilituma jumla ya Sh20 milioni kwa akaunti ya Gavana kwa kuziwezesha kupata zabuni hizo za jumla ya Sh365 milioni, dai ambalo Sonko amepinga vikali.

Kulingana na Bw Sonko, pesa hizo zilitumwa kwa akaunti yake na mfanyabiashara kwa jina Jamal, kabla yake kuingia afisini kama Gavana na “zilihusiana na biashara nyingine wala sio masuala ya zabuni ya uzoaji taka.”

“Pesa hizo zilitumwa kwa akaunti yangu mnamo Aprili 7, 2017 kabla yangu kuwa Gavana wa Nairobi. Jamal ni rafiki yangu na pesa hizo zilitokana na biashara nyingine ambayo tulifanya naye,” akasema.

Wasiwasi

Lakini Alhamisi Bw Sonko, ambaye alionekana mwenye wasiwasi alisema hivi: “Ikiwa sitapatikana na makosa nitaendelea na kazi yangu. Lakini ikiwa itabainika kuwa nina kosa basi nitaubeba msalaba wangu na kuondoka afisini ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi.”

“Lazima tuendeleza vita dhidi ya ufisadi. Na hatuwezi kudai kufanya hivyo huku tukisalia afisini baada ya kushtakiwa. Kwa hiyo huo ni msalaba nitabeba pekee yangu kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi vinavyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta,” Bw Sonko akaongeza.

Tangu alipoingia mamlakani kama Gavana wa Nairobi, Sonko amejidhihirisha kama kiongozi asivumilia sakata za ufisadi. Amekuwa akiwapiga kalamu mawaziri wake na maafisa wengine wa serikali wanaoshukiwa kushiriki uovu huo.