Habari MsetoSiasa

Sonko ashtakiwa na bwanyenye anayedai kuchafuliwa jina

April 11th, 2019 2 min read

NA ERICK WAINAINA

MVUTANO kati ya Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko na bwanyenye, Mike Maina, ambaye anamiliki hoteli ya Marble Arch, sasa umeishia mahakamani, tajiri huyo akidai Bw Sonko alimharibia jina.

Bw Maina ameshtaki kampuni ya Royal Media Services kwa kumpa gavana huyo jukwaa la kumtusi na kumharibia jina kupitia kipindi cha Jeff Koinange Live kilichopeperushwa Januari 13, 2019. Bw Sonko pia ametajwa kwenye kesi kama mshtakiwa.

Tajiri huyo jana alipata amri kutoka kwa Jaji Cecili Githua wa Mahakama ya Milimani inayozuia kampuni hiyo kuchapisha au kutangaza habari zozote kuhusu kesi hiyo hadi pale itakaposikizwa Mei 20, 2019.

Bw Maina pamoja na kampuni zake mbili Marble Ach Hotel na Muthithi Investment, ndiyo waliwasilisha kesi hiyo huku ikidaiwa utata kati yake na Bw Sonko ulisababishwa na ubomoaji wa makazi katika eneo la Nyama Villa, mtaa wa Kayole. Bw Maina alipanga kujenga nyumba ya kisasa ya mabilioni ya fedha.

Hata hivyo, Royal Media Services na mtangazaji Jeff Koinange, wamejitetea wakisema Bw Sonko ndiye anafaa kuwajibikia kesi hiyo kisheria, na kudai Bw Koinange alieleza wazi wakati wa kipindi hicho kuwa matamshi ya gavana yalikuwa ya kibinafsi wala hayakuwakilisha msimamo wa runinga ya Citizen.

Kupitia wakili wake Njenga Njehia, Bw Maina anadai matamshi ya gavana yamemvunjia heshima, kumletea aibu na kuwafanya marafiki zake wamdhihaki.

Hata hivyo, Bw Koinange na mwajiri wake wamejitetea wakisema kipindi hicho kilipeperushwa kwa nia nzuri kwa kuwa kililetwa moja kwa moja na kilizungumzia masuala yenye umuhimu kwa umma.

Pia wamedai Bw Koinange alisisitiza sana mwanzo wa kipindi kuwa matamshi yoyote yanayotolewa na wanaohojiwa si ya chombo hicho cha habari bali ya wageni wenyewe.

“Kwa hakika mshtakiwa wa pili (Koinange) na wa kwanza(Royal Media) hawafai kulaumiwa kwa matamshi ya Gavana Mike Sonko. Kwa hivyo anayefaa kugharimia kesi na uwajibikaji kutokana na kipindi cha JK Live kilichopeperushwa Januari 23, 2019 ni Gavana Mike Sonko,” washtakiwa walieleza katika jibu lao kortini.

Ombi la awali la Bw Maina kortini hata hivyo lilisema Bw Koinange alifahamu matamshi ya Bw Sonko yalikuwa ya kumharibia jina lakini wakaendelea kumpa nafasi .