Habari Mseto

Sonko ashtakiwa upya

September 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kesi za ufisadi Alhamisi ilitupilia mbali ombi la Gavana wa Nairobi Mike Sonko kupinga akishtakiwa upya katika kesi ya kula njama za ulaghai wa Sh14milioni.

Kufikia sasa Sonko anakabiliwa na kesi tatu za ufisadi wa Sh357m, Sh14m na Sh10m. Amezikanusha zote na yuko nje kwa dhamana.

Katika kesi ya jana alikana kupokea Sh8.4m akijua zimepatikana kwa njia haramu kutoka kwa kampuni ya Yiro iliyopewa kandarasi ya ukodishaji kaunti ya Nairobi mashine za kufanya kazi mbali mbali.

Hakimu mwandamizi Peter Ooko alisema ombi la Bw Sonko kupinga Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) asimfungulie mashtaka mapya halina mashiko kisheria.

Bw Ooko alisema sheria na katiba zinamruhusu DPP kufanyia marekebisho mashtaka dhidi ya Bw Sonko.

“ Hii mahakama haiwezi kupinga ombi la DPP kuwasilisha mashtaka mapya dhidi ya gavana huyu mradi hakuna ushahidi mpya utakaowasilishwa,” alisema Bw Ooko.

Hakimu alisema DPP alidokeza hatawasilisha ushahidi upya katika kesi hiyo Bw Sonko alishtakiwa mnamo Desemba 9 2019.

DPP kupitia kwa viongozi wa mashtaka Bw Wesley Nyamache alisema cheti cha mashtaka kilichowasilishwa kortini hakijafafanua kama inavyotakiwa kisheria kueleza jinsi makosa yalivyotendeka.

Hakimu alisema tayari ushahidi wote umekabidhiwa Sonko anayeshtakiwa pamoja na Fredrick Odhiambo almaarufu kama Fred Oyugi na ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya Yiro Enterprises.

Mshtakiwa mwingine ni Antony Otieno Ombok almaarufu kama Jamaal na aliyepia mmiliki wa kampuni ya ROG Securities.

Wote walikanusha mashtaka ya kula njama za kuifilisi kaunti ya Nairobi Sh14milioni kupitia kwa benki ya Equity kutokana na ukodishaji wa mitambo ya utengenezaji barabara na uchimbuaji mchanga.

Sonko alikanusha kupokea Sh8.4milioni akijua zimepatikana kwa njia ya uhalifu.

Sonko anawakilishwa na mawakili Cecil Miller na George Kithi..

Kesi itaanza kusikizwa Septemba 21,2020.