Habari MsetoSiasa

Sonko ashtuka kugundua hana mamlaka

April 7th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

ZAIDI ya wafanyakazi elfu sita wa Kaunti ya Nairobi, jana walikabidhiwa barua za uhamisho zinazowaelekeza wanakopaswa kuhudumu chini ya usimamizi mpya wa jiji la Nairobi (NMS).

Hii ni licha ya Gavana Mike Sonko na baadhi ya wakuu wa wafanyakazi kupinga shughuli hiyo iliyoendeshwa katika uwanja wa Uhuru Park na kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NMS Jenerali Mohammad Badi.

Bw Mbadi aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kusimamia NMS, ambayo ilitwaa baadhi ya majukumu ya kaunti yaliyohamishwa hadi serikali kuu ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Maelfu ya wafanyakazi walijitokeza Uhuru Park huku askari wa kitengo cha GSU wakishika doria na kutoa ulinzi mkali.

Mnamo Ijumaa wiki jana, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) iliwataka wafanyakazi 6,052 wa kaunti wafike mbele ya NMS ili wapokezwe barua za kuwaeleza majukumu yao mapya na afisi wanazopaswa kufanyia kazi.

Akipinga agizo hilo, Bw Sonko aliwataka wafanyakazi wasijitokeze kwa shughuli hiyo, akisema ilikuwa ikikiuka marufuku iliyowekwa na serikali dhidi ya kuandaliwa kwa mikutano inayohusisha mikusanyiko ya watu kutokana na janga la virusi vya corona.

Bw Sonko alidai kwamba kulikuwa na baadhi ya watu katika Ikulu ya Rais ambao walikuwa na nia ya kuvuruga uongozi wake.

Alidai waajiriwa wote wa kaunti wapo chini ya Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti ya Nairobi pekee wala sio PSC.

Jenerali Badi hata hivyo alipuuza madai ya gavana huyo, akisema hati iliyosainiwa katika Ikulu ya Nairobi, ilimpa mamlaka ya kusimamia majukumu yote yaliyohamishwa hadi serikali kuu.

“Nilichukua usukani Machi 18, 2020 baada ya Bw Sonko kutia saini stakabadhi za kuhamisha majukumu manne makuu. Bunge la kaunti pia liliidhinisha kuhamishwa kwa wafanyakazi na magari yao ili wawe chini ya NMS,” akasema Bw Badi.

Afisa huyo aliongeza kwamba shughuli hiyo itaendelea hadi Aprili 10,2020 na kufikia wakati huo watakuwa wamewakabidhi wafanyakazi wengine 3,000 barua zao.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi naye alisema mkutano utaandaliwa wiki hii kati ya viongozi wa Muungano wa wafanyakazi na NMS ili kusikiza malalamishi ya wafanyakazi wasioridhishwa na shughuli hiyo.