HabariSiasa

Sonko ataponea?

December 11th, 2019 2 min read

RICHARD MUNGUTI na WANDERI KAMAU

HATIMA ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko, iwapo ataendelea kushikilia wadhifa wake itajulikana Jumatano wakati Mahakama ya Milimani, Nairobi itaamua kama anastahili kuachiliwa kwa dhamana.

Inasubiriwa kuonekana kama Sonko, ambaye alikanusha mashtaka ya ufisadi Jumatatu pamoja na washukiwa wengine, atafuata mkondo wa mwenzake wa Kiambu, Ferdinand Waititu na Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal Kasaine waliokatazwa na korti kuingia afisini mwao waliposhtakiwa kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Masaibu ya Bw Sonko yamezidishwa na mashtaka mengine mengi yanayomkodolea macho, yakiwemo madai ya kuvurutana na polisi alipokuwa akikamatwa Voi mnamo Ijumaa iliyopita, na madai ya kutoroka Gereza la Shimo la Tewa mnamo 1998.

Mnamo Jumatatu, mawakili wake walikuwa wameiomba mahakama kuchukulia kesi yake kwa njia tofauti na zile za Kaunti za Kiambu na Samburu, wakidai Nairobi ni kaunti ya kipekee kwa kuwa haina hata naibu gavana ambaye atashikilia shughuli za utawala endapo Sonko atakatazwa kukanyaga guu afisini.

“Madai eti Sonko anasakwa kwa makosa ya kutoroka gerezani hayana msingi wowote na hayana mashiko kisheria kwa kuwa aliachiliwa huru na Mahakama Kuu 2000,” alisema mmoja wa mawakili wake, Bw Cecil Miller.

Matukio haya yameweka Kaunti ya Nairobi katika hatari ya kiuongozi.

Ingawa Katiba inaweka kaunti chini ya uongozi wa naibu gavana ikiwa gavana hayupo, Bw Sonko hajamteua naibu wake hadi sasa tangu Bw Polycarp Igathe ajiuzulu wadhifa huo mnamo Januari 2018.

Kulingana na Katiba, Spika ndiye anapaswa kuongoza kaunti, ikiwa gavana na naibu gavana hawapo kwa sababu ya kifo, kujiuzulu, kung’atuliwa mamlakani kisheria au kuhukumiwa kwa mashtaka ya uhalifu.

Anafaa kushikilia mamlaka hayo kwa siku sitini kabla uchaguzi mpya wa ugavana uitishwe. Lakini sheria haifafanui wazi kama mwelekeo huu unastahili kufuatwa kabla gavana kuhukumiwa ndiposa kuna wasiwasi kuhusu usimamizi wa jiji.

Kulingana na kipengele 192 (c) cha Katiba, huenda Rais Uhuru Kenyatta akalazimika kutumia mamlaka yake kuvunja serikali ya kaunti hiyo ambapo baadaye kutaandaliwa uchaguzi mdogo.

Kipengele hicho kinampa Rais mamlaka ya kuvunja serikali ya kaunti katika dharura inayotokana na vita au hali zingine tofauti.

Kulingana na Naibu Kiongozi wa Wengi katika Seneti Prof Kithure Kindiki, huenda hali ilivyo Nairobi ikajumuishwa “katika hali zingine” kwani hakuna vita nchini wala hakuna malumbano ya kindani miongoni mwa viongozi katika kaunti hiyo.

“Ikiwa Rais Kenyatta atafuata mwelekeo huo, sheria inaeleza kuwa serikali hiyo itavunjwa kwa muda wa miezi mitatu, ambapo baadaye kutaandaliwa uchaguzi mdogo,” akasema Prof Kindiki, ambaye pia ni seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi.

Vile vile, huenda Bw Sonko akashinikizwa kumteua Naibu Gavana kwa haraka, ambaye atahojiwa na kupitishwa na Bunge la Kaunti.

Jana, ilibainika Sonko alipelekwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu ya majeraha aliyodai alipata alipopigwa na polisi.

Sonko aliondolewa kutoka gereza kuu la Kamiti na kupelekwa KNH kwa ushirikiano wa maafisa wa idara ya magereza, afisa mkuu wa polisi anayechunguza kesi yake, na mawakili wake wakiongozwa na George Kithi.

Kufikia saa kumi alasiri jana, Bw Kithi na watu wa familia ya Sonko walikuwa bado wanashughulika alazwe KNH.

Jumatatu alasiri, Hakimu Douglas Ogoti aliamuru Sonko azuiliwe katika gereza lililo na kliniki ambako anaweza kupokea matibabu na akizidiwa “apelekwe KNH” kwa matibabu maalum.

Kwa mujibu wa ripoti ya Dkt Esther Nekesa Wafula wa hospitali ya MP Shah aliyempima Sonko Jumamosi, alipendekeza afanyiwe ukaguzi zaidi ibainike ikiwa amevunjwa mbavu.