Habari

Sonko atetea hatua yake kuwasimamisha kazi baadhi ya maafisa

November 19th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amesema ataendelea kuwafuta kazi maafisa wazembe na mafisadi, licha ya hatua hiyo kukosolewa.

Sonko amesema wafanyakazi atakaosaza ni wanaofanya kazi kwa uwazi na uaminifu.

Kauli yake imejiri siku moja baada ya kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, kaunti ya Nairobi.

Tangu achaguliwe gavana 2017, Sonko amefanya mabadiliko ya baraza hilo mara sita.

“Mtu yeyote mzembe na mfisadi nitamsimamisha kazi. Lazima tufanyie watu kazi waliyotuchagua tuwe ofisini,” gavana Sonko akasema mnamo Jumatatu.

Akionekana kukerwa na baadhi ya wakosoaji wake, alisema kuna magavana wanaofuta kazi maafisa wao ilhali hawakosolewi.

“Ninashangaa Hassan Joho (Mombasa) na Anyang’ Nyong’o (Kisumu) wamefuta karibu baraza lote, watu hawaongei, lakini Sonko wanaongea,” akalalamika.

Gavana huyo alitetea hatua ya kutimua baadhi ya maafisa akisema kwamba wamehusika kwenye sakata za ubadhirifu wa fedha, mali ya umma na hata utumizi mbaya wa ofisi. Alishangaa wakosoaji wake kuendelea kumchimbua, akidai hakuna aliyeenda kortini kusimamisha hatua yake.

Charles Kerich, aliyesimamia wizara ya fedha na Mohammed Dagane, CEC wa mazingira ni baadhi ya maafisa waliosimamishwa kazi Septemba 2019 na gavana huyo. Itakumbukwa kwamba aliyekuwa naibu gavana Nairobi, Polycarp Igathe mapema 2018 alijiuzulu kwa madai ya kushindwa kufanya kazi na Bw Sonko.

Wiki iliyopita, tume ya maadili na kupambana na ufisadi, EACC iliwahoji mawaziri wa Bunge la Kaunti ya Nairobi kwa tuhuma za ufisadi.

Kuhojiwa

Gavana Sonko pia amehojiwa mara kadhaa na EACC kwa madai yayo hayo.

Hata hivyo, anasema baadhi ya maafisa wa tume hiyo wanamuandama kwa kile anataja kama kuziba mianya yote ya ufisadi Nairobi.

Alisema kuna maafisa wa EACC wanaohusishwa na unyakuzi wa ardhi Nairobi, hivyo basi wanajaribu juu chini kumng’atua. Alitoa tetesi hizo akirejelea bomoabomoa ya majengo haramu katika hiyo, hapo awali.

“Nitaendelea kubomoa majengo haramu, ukifuata sheria sina shida na wewe. Baadhi ya wenye majengo hayo Nairobi wana ushawishi mkuu serikalini, na hawanibabaishi,” akasisitiza gavana huyo.