Habari Mseto

Sonko ateua naibu, MCA wakijadili hatima yake

January 7th, 2020 2 min read

COLLINS OMULO na LEONARD ONYANGO

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, amemteua Bi Anne Kananu Mwenda kuwa naibu wake.

Uamuzi huo ulichukuliwa siku moja tu kabla madiwani wa kaunti hiyo kukutana leo kushauriana kuhusu hatima ya utawala wa Bw Sonko aliyeamrishwa kutoingia afisini hadi kesi yake ya ufisadi ikamilike.

Ijapokuwa haikufahamika mara moja kama hatua ya Bw Sonko ilikiuka agizo lililomkataza kurejea afisini, alisema alifanya hivyo ili shughuli za kaunti ziendelee mbele na amejitolea kutii maagizo ya mahakama.

“Ninaomba bunge la kaunti liharakishe kumhoji naibu gavana mteule ili aajiriwe kwa msingi wa Sheria za Serikali ya Kaunti,” akasema kwenye taarifa.

Bi Kananu alikuwa Afisa Mkuu wa kusimamia majanga katika utawala wa Gavana Sonko.

Madiwani leo watahudhuria mkutano wa Kamukunji ambao utatoa mwelekeo wa kuandaliwa kwa kikao maalum mnamo Alhamisi huku ikikisiwa mswada wa kutokuwa na imani na gavana huyo huenda ukawasilishwa bungeni siku hiyo.

Mkutano huo unatarajiwa kuandaliwa kwenye majengo ya kaunti na utahudhuriwa na madiwani wote 122 pamoja na Spika Beatrice Elachi, lengo kuu likiwa ni kuangazia matatizo ambayo yamezonga kaunti tangu Bw Sonko azuiwe kuingia afisini na mahakama mwezi uliopita.

Kufuatia hatua ya Jumatatu, huenda suala la uteuzi wa naibu gavana pia likapewa kipaumbele katika mkutano huo wa madiwani.

Madiwani wa ODM wamekuwa wakieleza wazi nia ya kutaka Bw Sonko atimuliwe, wakidai kwamba kuzuiwa kukanyaga afisini pia kunamzuia kutekeleza majukumu yake kikamilifu kama gavana.

Kwa upande mwingine, Bi Elachi na baadhi ya madiwani wa Jubilee wamekuwa wakikataa nia ya kuandaliwa kwa kikao cha kumbandua Bw Sonko, wakisema kuwa bado wanasuburi ushauri wa Mwanasheria Mkuu pamoja na Mahakama ya Juu.

Ingawa hivyo, sasa mrengo huo unaonekana kukata tamaa ya kusubiri mwelekeo huo baada ya Bi Elachi kuthibitisha kwamba atachapisha kwenye gazeti rasmi wito wa kuandaliwa kwa kikao hicho maalum Januari 9, 2019, saa nane na nusu mchana.

Kamukunji yasitishwa

Kamukunji hiyo imeitishwa na Bi Elachi kwenye barua kwa viongozi wa vyama vya Jubilee na ODM.

“Ajenda itatolewa wakati wa mkutano huo,” akaongeza Bi Elachi kwenye barua kwa kiongozi wa wengi Charles Thuo na mwenzake wa wachache David Mberia. Viranja wa wengi na wachache June Ndegwa na Peter Imwatok pia walinakiliwa kwenye barua iliyoandikwa Januari 3, 2019 inayopendekeza kuandaliwa kwa kamkunji hiyo.

“Niliona ni vyema madiwani wawe na kamkunji kabla ya kuandaliwa kwa kikao spesheli. Bunge lipo likizoni lakini wawakilishi wadi wametiwa hofu na hali ya sasa ya kaunti. Hili si suala la mtu binafsi, ODM au Jubilee bali watu wa Nairobi,” akasema Bi Elachi.

Kwa upande wa Mabw Mberia na Thuo walithibitisha kwamba wawakilishi wadi wote wa ODM na Jubilee watahudhuria kamukunji hiyo.

“Tunataka kuamua suluhisho ya utawala wa Nairobi kwa sababu tusipofanya hivyo, wapigakura hawatawahi kutusamehe,” akasema Bw Mberia.