Habari

Sonko atolewa pumzi

November 2nd, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

MASAIBU ya Gavana wa Nairobi, Mike Sonko yanaendelea kuongezeka hata zaidi baada ya kukabiliwa na kibarua kingine cha kujitetea dhidi ya madai kuwa alitoa habari za uongo ili kuruhusiwa kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Katika hatua inayoweza kumzima zaidi gavana huyo mwenye mbwembwe za kila aina, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), inadai imepokea habari kwamba Bw Sonko alitoa habari za kupotosha kwenye fomu ya kiapo kuelezea rekodi zake za uhalifu kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.

Baada ya kupata habari hizo, Gavana Sonko alisema anawindwa kwa kutimua wafanyabiashara walaghai katika serikali ya Kaunti ya Nairobi ingawa mwenyewe amechunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Hii imemfanya kuingiwa na baridi na kuacha vituko alivyotambuliwa navyo siku zake za kwanza mamlakani akiwa gavana alipokuwa akivamia ofisi za idara tofauti za kaunti na kurekodi wafanyakazi na kuwasimamisha baadhi kazi.

Alikuwa akiwahusisha maafisa hao na ufisadi, madai ambayo siku za hivi majuzi yamekuwa yakimuandama.

EACC imemwalika kufika mbele ya maafisa wake Jumanne ijayo, Novemba 5 kuandikisha taarifa kuhusu fomu inayodai alijaza 2017.

“Tume hii inachunguza madai kwamba ulitoa habari za uongo kwenye fomu uliyojaza mwenyewe mnamo Machi 9 2017 na kuwasilisha kwa tume,” inasema barua ya Afisa Mkuu Mtendaji Twalib Mbarak kwa Bw Sonko.

EACC ina mamlaka ya kufuatilia maadili ya viongozi na rekodi za uhalifu za maafisa wa umma na wanaotaka kushikilia viti hivyo.

Inasemekana kuwa alidanganya kwamba hakuwa na kesi mahakamani wakati wa kujaza fomu hiyo ilhali alikuwa na kesi 10 zilizokuwa zikiendelea wakati huo.

Hii itakuwa mara ya pili ya Bw Sonko kuhojiwa na tume hiyo.

Mnamo Septemba, maafisa wa EACC walimhoji kuhusiana na madai ya ufisadi katika utoaji wa zabuni ya uzoaji taka katika serikali ya kaunti.

Gavana huyo analaumu baadhi ya watu wenye ushawishi kumhangaisha kwa sababu ya mageuzi makubwa anayotekeleza katika serikali ya kaunti.

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Facebook, Bw Sonko alidai madai hayo hayana msingi akisema, tume hiyo ilimuidhinisha kugombea viti tangu 2010 alipogombea kiti cha eneobunge la Makadara kwa mara ya kwanza.

“Kwa nini DCI ( Idara ya upelelezi wa Jinai) iliniidhinisha kugombea ubunge 2010, useneta (2013) na ugavana(2017)?” alihoji Bw Sonko.

Kulingana na Bw Sonko, madai hayo yanalenga kumtisha ili aache kufuatilia masuala yanayoathiri umma.

Gavana huyo alisisitiza kwamba haogopi kuangazia tabia yake kabla ya kuwa kiongozi na kuwataka wanaomwandama wakome kutumia rekodi yake ya zamani kumhukumu.

“Mara kwa mara nimekuwa nikikiri maisha yangu ya awali na kusisitiza kuwa hayafai kuathiri kujitolea kwangu wakati huu na azima yangu siku sijazo kwa sababu hakuna hali ambayo ni ya kudumu kwa kuwa kila kitu kinawezekana kupitia Mungu,” Bw Sonko alisema.

Bw Sonko amekuwa akitangaza wazi kuwa aliwahi kufungwa jela mara kadhaa kabla ya kujiunga na siasa.

Kesi

Akiwa mbunge wa Makadara, alikabiliwa na kesi kadhaa za uhalifu, kuzua ghasia na kushambulia hata maafisa wa polisi.

Alisuluhisha baadhi ya kesi nje ya mahakama. Licha ya kesi hizo, umaarufu wake uliongezeka kwa kutetea mwananchi wa kawaida na akashinda useneta kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 kabla ya kuchaguliwa gavana wa pili wa Nairobi 2017.

Masaibu ya Sonko yanajiri wakati Bunge la kaunti ya Nairobi limekumbwa na mzozo wa uongozi ambao anadaiwa kuhusika.

Mwezi jana, alimwandikia barua Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee akitaka kiongozi wa wengi Abdi Guyo atimuliwe.

Bw Guyo amekuwa akipinga kurejea kwa Spika Beatrice Elachi ambaye alikuwa ameondolewa mamlakani.

Duru zinasema Sonko anahisi Bw Guyo amekuwa akitumiwa na watu wenye ushawishi kuchochea masaibu yake katika EACC.