Sonko augua akiwa rumande, alazwa hospitalini

Sonko augua akiwa rumande, alazwa hospitalini

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, amelazwa hospitalini saa chache kabla ya kufikishwa korti ya Kiambu ambako ameshtakiwa kwa madai ya kushambulia na wizi wa mabavu.

Wakili wake John Khaminwa alisema Bw Sonko alikimbizwa katika hospitali ya Nairobi kutoka rumande baada ya kuugua.

Ingawa wakili huyo hakufichua anachougua mwanasiasa huyo ambaye pia anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi, duru zilisema kwamba alikuwa na maumivu ya tumbo.

Sonko alitarajiwa kufikishwa katika mahakama ya Kiambu Jumanne asubuhi na katika mahakama ya Kahawa baadaye adhuhuri.

Wakili Khaminwa alisema kwamba watajaribu kufikia Sonko kortini alivyoagizwa.

Maafisa wa upelelezi wa uhalifu wanaema kwamba wana habari Sonko alikuwa akihusika na vitendo vya kigaidi, Wanaomba mahakama iwaruhusu wamzuilie kwa siku 30 ili wakamilishe uchunguzi.

Wasaidizi tisa wa Bw Sonko pia wamekamatwa kuhusiana na madai hayo.

Sonko amekuwa akilalamika kuwa maisha yake yamo hatarini akidai maafisa wa polisi walijaribu kumdunga sumu akiwa seli.

Upande wa mashtaka umeomba asiachiliwe kwa dhamana ukidai anaweza kutoroka alivyofanya 2001 katika kesi iliyomkabili Mombasa.

Bw Sonko amekanusha madai hayo.

You can share this post!

Omanga asema haendi popote

Shule ya Mwiki kupanuliwa