Habari Mseto

Sonko awaita majambazi awape ajira

November 21st, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ameamua kutumia mbinu isiyo ya kawaida kupigana na uhalifu Jijini Nairobi, baada ya kuwataka wakora wote kumtafuta katika ofisi yake ili awape kazi.

Gavana Sonko katika ujumbe wake anawataka wakora wanaotumia bunduki na silaha nyingine kuwahangaisha wakazi na wafanyabiashara wa jiji kusalimisha silaha hizo kwa mamlaka zinazofaa, kisha waje mezani kwa mazungumzo namna atawapa kazi.

Akiapa kuwa hatarudi nyuma katika vita dhidi ya uhalifu, aliwaonya watu wanaojihusisha na visa hivyo kuwa wasipowacha siku zao zinahesabiwa, ujumbe wake ukija siku chache baada ya polisi kuua washukiwa saba wa uhalifu wikendi iliyopita.

“Hakuna kurudi nyuma kwenye vita dhidi ya uhalifu wa silaha Jijini na maeneo ya karibu. Wale wako na bunduki kinyume na sheria pelekeni kwa Chifu wa eneo lako, kituo cha polisi cha karibu, ofisi ya MCA ama mniletee kwa ofisi yangu. Kama ni kazi njooni tukae tuelewane badala ya kuua watu wasio na hatia,” Bw Sonko akasema kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumatatu jioni.

Alisisitiza kuwa ni heri awaajiri kazi wapate la kufanya, badala yao kwenda wakiua watu kiholela na kusababisha utovu wa usalama jijini.

Vilevile, gavana huyo aliwazawadi Sh500, 000 maafisa wa polisi ambao waliangamiza washukiwa hao saba katika visa viwili tofauti Jijini, ambapo washukiwa waliripotiwa kukabiliana na polisi.

“Tulitenga siku saba kwa watu wa magenge yaliyo na silaha kuzisalimisha na kuwacha kuwahangaisha wakazi wa Nairobi mara moja. Baadhi yao walitii lakini wengine wakakaidi amri,” akasema gavana huyo.