Habari

Sonko awalilia Rais, Raila asing’atuliwe

November 29th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Mbuvi Sonko amenyenyekea kwa Rais Uhuru Kenyatta huku akikumbatia mbinu mbalimbali ili kujinusuru dhidi ya kung’atuliwa enzini na madiwani.

Madiwani 86 kutoka vyama vya ODM na Jubilee tayari wametia saini hoja ya kumbandua Bw Sonko, japo nafuu kwake ni mgawanyiko ambao umeanza kujitokeza kati ya madiwani hao kabla ya hoja ya kumtimua kuwasilishwa.

Duru zilieleza Taifa Jumapili kwamba seneta huyo wa zamani wa Nairobi ameanza kuweka mikakati maridhawa kuhakikisha kuwa hoja hiyo haifaulu.

Bw Sonko tayari ametuma wandani wake kumtetea kwa Rais Uhuru Kenyatta, ikidaiwa sasa yuko tayari kulegeza msimamo kuhusu bajeti ya kaunti ya 2020/21.

Msimamo wake mkali kuhusu bajeti hiyo umelinyima Shirika la Huduma ya jiji la Nairobi (NMS) fedha za kufadhili miradi mbalimbali iliyoanzishwa na mkurugenzi wa shirika hilo Meja Jenerali Mohammed Badi.

Pia, Bw Sonko alikutana na kinara wa ODM Raila Odinga ambapo inadaiwa alimrai azungumze na madiwani wa chama hicho katika Bunge la kaunti yake wasiunge mkono hoja ya kumbandua.

Gavana huyo anawahitaji zaidi ya madiwani 41 kati ya 122 wote kumuunga mkono mradi tu hoja hiyo isiungwe mkono na idadi inayohitajika ya theluthi mbili ambayo ni madiwani 82.

Madiwani 27 walipiga kura ya kuunga mkono utetezi wake wa kupinga bajeti ya Sh37.5 bilioni, hilo likimaanisha kuwa sasa atahitaji madiwani wengine 14 ili kufaulu kuangusha hoja ya kumtimua.

Aidha, mbinu ya mwisho anayolenga kutumia Bw Sonko ni kuwafikia maseneta kumpa jukwaa zuri la kujitetea na kuamrisha aendelee na majukumu yake iwapo hoja ya kumtimua itapitishwa wiki hii.

Baadhi ya madiwani wanaomuunga mkono Bw Sonko tayari wameapa kupinga hoja hiyo wakisema msingi wake hauna mashiko na hautoshi kumwondoa afisini.

“Ni kweli Bw Sonko alikutana na Bw Odinga pamoja na baadhi ya madiwani wa ODM wanaopinga kubanduliwa kwake. Mkutano huo ulikuwa wa nia njema na gavana ana uhakika atajinasua,” akasema diwani mmoja ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

Diwani mwengine alisema mbunge huyo wa zamani wa Makadara amelegeza msimamo na sasa yuko tayari kutia saini mswada wa kuidhinisha bajeti ili Sh27.1 bilioni zielekezwe kwa NMS naye asalie na Sh8.4 bilioni kuendesha serikali yake.

Hata hivyo, Kiranja wa Wachache Peter Imwatok anashikilia kuwa muda wa Bw Sonko kama gavana wa Nairobi umekwisha na hoja ya kumtimua itapitishwa liwalo liwe.

“Nataka kupuuza madai kwamba ni Rais aliyemwokoa Bw Sonko hoja ya kumtimua ilipokosa kuwasilishwa bungeni mnamo Februari. Wakati huo korti ndiyo iliyotuzuia kwa kutofuata sheria lakini sasa tumetimiza kila hitaji na liwalo liwe Sonko anaenda nyumbani,” akasema diwani huyo wa Makongeni.

Hata hivyo, diwani wa Imara Daima Kennedy Obuya alidai kiongozi wa wachache Michael Ogada na Bw Imwatok wanatishia madiwani na kuwalazimisha kuunga hoja dhidi ya Bw Sonko.