Habari Mseto

Sonko awaokoa walioshindwa kulipa bili za hospitali

April 7th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, Jumapili aliamuru usimamizi wa hospitali zote za kaunti kuwaachilia wagonjwa wanaozuiliwa kutokana na malimbikizi ya gharama za matibabu.

Bw Sonko alisema serikali yake kupitia wizara ya fedha ya kaunti, itagharimia fedha zote wagonjwa hao wanadaiwa baada ya kukadiria kiasi cha jumla wanachotakikana kulipa.

“Namwaamuru waziri wangu wa fedha kuchunguza na kutathmini kiasi cha fedha wagonjwa wanaoendelea kuzuiliwa wanadaiwa ili serikali yangu iweze kuzilipa mara moja. Pia naamuru hospitali zote zilizoko chini ya kaunti kuwaachlia mara moja wagonjwa wote wanaoendelea kuzuiliwa kwa kutokamilisha ada za matibabu,” akasema Bw Sonko.

Gavana huyo alisema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kutenda Wema Duniani, hafla iliyoandaliwa mbele ya afisi yake ya City Hall.

Akiwa ameandamana na baadhi ya mawaziri, Bw Sonko aliahidi kuendeleza matendo mema kwa wasiobahatika katika jamii jinsi ambavyo amekuwa akifanya. Gavana huyo amekuwa akishutumiwa na badhi ya viongozi kwa kukimbilia kutoa msaada kwa watu katika maeneo mengine ya nchi na kusahau wakazi wa kaunti ya Nairobi.

Majuzi Bw Sonko alikabiliana na Mbunge Mteule Maina Kamanda katika mtandao wa Twitter baada ya Bw Kamanda kumkejeli kwa kukimbilia kutoa msaada kwa wakazi wa Turkana wanaokumbwa na baa la njaa badala ya kushughulikia changamoto chungu nzima zinazokumba kaunti ya Nairobi.

“Mimi nitaendelea kutenda mema jinsi nimekuwa nikifanya katika maisha yangu kwa kuwa vitendo vyangu vinalenga maskini wala si vya kujionyesha. Ni jukumu la viongozi kuhakikisha hakuna mwanachi anayeangamia kutokana na baa la njaa na pia kuweka mikakati kuepuka maafa ya njaa siku zijazo,” akaongeza Bw Sonko.

Aidha kinara huyo wa kaunti alitaka wanaojiweza kusaidia wananchi maskini badala ya kujikita katika kuunda mali na kuongezea utajiri wao. Alitoa mfano wa mataifa kadhaa duniani ambako pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa mno.

Kongamano kubwa la Matendo Mema Duniani linatarajiwa kuandaliwa mjini Nairobi mwezi Agosti mwaka huu. Hafla ya jana ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Umoja wa Kimataifa(UN), Shirika la Msalaba Mwekundu na wawakilishi kutoka makao ya kuwatunza watoto.