Habari Mseto

Sonko, Badi wazidi kuvutania ukusanyaji kodi

August 10th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

MVUTANO wa Gavana wa Nairobi Mike Sonko dhidi ya Mkurugenzi wa Shirika la Huduma la Nairobi (NMS) Mohammed Badi, sasa unaelekea kuwakanganya wakazi wa Nairobi kuhusu ulipaji kodi na kutishia kulemaza utoaji huduma.

Gavana huyo ameibua mzozo mpya kwa kuzindua mfumo tofauti wa kukusanya ushuru, baada ya NMS kuzindua mwingine hivi majuzi.

Wiki iliyopita, NMS ilitangaza mfumo mpya wa kulipia ushuru kupitia nambari, *647# kwa wakazi wanaotaka huduma mbalimbali.

Serikali ya Bw Sonko nayo sasa imewataka wakazi kulipa ushuru kupitia mtandao wa epayments.nairobi.go.ke, mfumo unaotayarishwa na National Bank.

Kulingana na serikali ya Bw Sonko, ni ada za maegesho ya magari pekee ambazo hawafai kutumia mfumo huo kulipia.

Utawala huo unasema, wanaotafuta vyeti za afya, leseni za biashara, kodi, ada za ardhi, masoko miongoni mwa nyingine wanafaa kutumia mfumo wa kaunti.

“Tembelea epayments.nairobi.go.ke, chagua huduma unayotaka kulipia kisha weka akaunti yako iwapo haihusu maegesho,” lilinasema tangazo ambalo serikali ya kaunti ya Nairobi inapanga kutoa kwa wakazi.

“Utapokea ujumbe kwenye simu yako kukutaka ulipe kupitia Mpesa. Aidha, unaweza kwenda kwa menu ya Mpesa, chagua Lipa na Mpesa, chagua unataka kulipa bili kisha uweke nambari ya biashara 367776 na nambari ya akaunti iliyo mtandaoni,” tangazo linaeleza.

Hii itazua mgongano na mfumo wa NMS ambao pia unatumia mtandao kukusanya ushuru katika kaunti zikiwemo ada za maegesho, leseni za biashara, ada za ardhi, masoko na nyumba miongoni mwa huduma nyingine. NMS linashirikiana na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA).

Shirika hilo lilisema kwamba kwa sasa mfumo huo unatumika katika majukumu yaliyohamishiwa serikali ya kitaifa lakini baadaye utatumiwa kwa huduma zote katika serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Mfumo wa kutumia nambari *235# ambao ulikuwa ukitumika tangu serikali ya kaunti ya Nairobi ilipovunja mkataba na kampuni ya JamboPay, hautakuwa ukitumika.

Hatua ya Bw Sonko inaendeleza mzozo kati ya viongozi hao wawili tangu NMS ilipobuniwa Machi kusimamia huduma za afya, uchukuzi, ujenzi, mipango na maendeleo miongoni mwa nyingine.

Mgogoro ulianza na kuhamishwa kwa wafanyakazi 6,000 wa serikali ya kaunti mnamo Aprili, kisha ukaendelea kuhusu bajeti ya ziada kabla ya viongozi hao kuanza kuzozania utekelezaji wa miradi ya maendeleo jijini kila mmoja akitaka kuhusishwa nayo.

Madiwani wa kaunti ya Nairobi sasa wanataka serikali ya kaunti kushirikiana na NMS kuweka sera ambayo itaidhinishwa bunge la kaunti kutoa mwongozo wa kuhamisha wafanyakazi kati ya ofisi hizo mbili.

Wanasema sera hiyo itakomesha mzozo katika ya ofisi hizo mbili kuhusu kuhamishwa kwa wafanyakazi wa Umma kutoka serikali ya kaunti hadi shirika la NMS.