Habari Mseto

Sonko na Sakaja wakabana koo

April 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko na Seneta wa Kaunti hiyo Johnstone Sakaja Alhamisi walijibizana mbele ya kamati moja ya seneti kuhusu suala la gavana huyo kuchelewesha uteuzi wa naibu wake.

Bw Sonko alimkaripia Bw Sakaja kwa kuwasilisha suala hilo katika bunge la seneti bila kwanza kumuuliza ili amwelezea sababu ya yeye kuchelewesha uteuzi huo miezi 15 baada ya kujiuzulu kwa Bw Polycarp Igathe.

Gavana huyo alitaja suala hilo kama lisilo na maana na akamlaumu Sakaja kwa kuliliibua na hivyo kupoteza”wakati wa maseneta wenzake”.

“Huyu Sakaja ni rafiki yangu na tulifanya kampeni pamoja chini ya mwavuli wa chama chetu cha Jubilee. Lakini iweje sasa analeta suala hili ambalo halina maana mbele ya seneti kabla kwamba kuzungumza nami ili apate ukweli wa mambo,” akafoka Bw Sonko.

“Hata juzi alinitumia picha ambazo tulipiga miaka miwil iliyopita tukiwa katika kampeni. Kwa hivyo, nashangaa kwamba huyu seneta anaweza kuleta suala hili mbele ya kamati hii,” Bw Sonko akaongeza.

Gavana huyo alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi kuelezea ni sababu ya kutoteua naibu wake, miezi 15 baada ya Bw Igathe kujiondoa.

“Hamna haja kuwaita maseneta kuja kushughulikia suala ambalo halina maana yoyote. Nilionyesha nia njema kwa kumteua Miguna Miguna lakini bunge la Kaunti ya Nairobi likakataa jina lake,” akasema.

“Na baadaye muungano wa NASA ukapendekeza majina ya Rahab Ndambuki na Jane Wangui. Baadaye Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju pia alinipigia siku akiniambia nishuriane zaidi. Kwa hivyo, nimekuwa nikishauriana kwa moyo wa handisheki,” Bw Sonko akasema.

Gavana huyo alidai kuwa Bw Sakaja anampiga vita kwa sababu anakimezea mate kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, Sakaja alikana madai hayo akisema hajawahi kutanga nia yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi.

“Silengi kiti chochote wakati huu. Langu ni kutekeleza wajibu wangu kama Seneta wa Nairobi kwa kuchunguza utendakazi wa serikali ya Nairobi. Wakati ukifika nitakuwa na haki ya kuwania kiti chochote ambacho nitapenda kwa sababu hiyo ni haki yangu ya kikatiba,” akasema Bw Sakaja.

Bw Sonko aliiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Laikipia John Kinyua kwamba kando na kuendelea kufanya mashauriano, hakuna sheria inayomlazimu kuteua naibu wake baada ya kipindi fulani.

“Sheria hiyo itakapotiwa sahihi na Rais Kenyatta, naapa mbele ya kamati hii kwamba nitateua naibu gavana baada ya sekunde moja,” Bw Sonko aeleza.