Habari

Sonko nje

December 18th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE maseneta Alhamisi usiku walipiga kura ya kuidhinisha hoja ya kumtimua afisini Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko baada ya kikao kilichoibua joto kali katika bunge hilo.

Joto hilo lilisababishwa na pingamizi kutoka kwa maseneta wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto, almaarufu, ‘Tangatanga’ waliolalama kuwa sheria na kanuni zilikiukwa wakati madiwani walipitisha hoja hiyo mnamo Desemba 3, 2020.

Maseneta 27 wa mrengo wa ‘Kieleweke’ walipiga kura ya NDIO na kuidhinisha mashtaka manne dhidi ya Sonko katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na madiwani 88 kati ya 122 wa bunge la Kaunti ya Nairobi.

Lakini maseneta 16 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walipiga kura ya LA huku nao maseneta Johnson Sakaja (Nairobi) na Mutula Kilonzo Junior (Makueni) wakisusia upigaji kura licha ya wao kuwa bungeni na kushiriki mjadala kuhusu hoja hiyo.

Naye Seneta wa Garissa Yusuf Haji hakuwepo kwa sababu anaugua ilhali Seneta wa Machakos Boniface Kabaka alifariki juzi.

Hoja hiyo ilikuwa imedhaminiwa na Kiongozi wa Wachache na Diwani wa Embakasi Michael Ogada mnamo Novemba 13.

Mashtaka dhidi ya Sonko kwenye hoja hiyo yalikuwa; ukiukaji wa Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya na kutenda uhalifu chini ya sheria za kitaifa.

Maseneta walipiga kura kwa kila shtaka, moja baada ya nyingine, ambapo maseneta 27 walikubaliana nayo na wengine 16 wakayakatalia mbali.

“Maana ya matokeo upigaji kura huu ni kwamba Gavana Mike Mbuvi Sonko wa Kaunti ya Nairobi ameondolewa afisini,” akasema Spika wa Seneti Kenneth Lusaka mnamo Alhamisi mwendo wa saa tano na dakika 20 za usiku baada ya kutangaza matokeo.

Hii ni baada ya mawakili wa bunge la Kaunti ya Nairobi na wale wa Sonko kutetea ushahidi waliokuwa nao kuthibitisha misimamo ya wateja wao katika kikao maalumu kilichodumu kwa siku mbili, Jumatano na Alhamisi.

Bw Sonko naye alipata fursa ya kujitetea dhidi ya madai hayo akisema kuwa hoja hiyo ilichochewa kisiasa kwa nia ya kumharibia jina na kuzika nyota yake katika ulingo wa siasa.

“Nawaomba waheshimiwa maseneta kutupilia mbali hoja hii kwa kando na kusheheni madai ya uongo na inachochewa na chuki kutoka kwa madiwani mafisadi ambao hawakufurahia kujitolea kwangu kupambana na ufisadi katika serikali yangu,” Sonko akasema katika taarifa yake ya mwisho.

Akijitetea, Sonko alikana madai kuwa alizima utoaji wa Sh197 milioni fedha za basari ya wanafunzi akisema alichukua hatua hiyo kuzima ufisadi ulioingizwa katika mpango huo, wahusika wakuu wakiwa madiwani na washirika wao.

Aidha, alikana kuwa bintiye Saumu Mbuvi, alitumia Sh800 milioni fedha za kaunti ya Nairobi katika ziara ya anasa jijini New York, Amerika akisema ziara hiyo ilifadhiliwa na serikali ya kitaifa kwa kima cha Sh4.3 milioni.

Hata hivyo, Sonko ana nafasi ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga kutimuliwa afisini au asubiri kuwania kiti hicho tena katika uchaguzi mdogo utakaoandaliwa ndani ya siku 60.

Hii ni kwa sababu kaunti ya Nairobi haina naibu gavana ambaye angeshikilia wadhifa huo, baada ya Polycarp Igathe kujiuzulu Januari 1, 2018.