Michezo

SoNy katika hatari ya kuondolewa KPL isipocheza leo Jumamosi

October 26th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Klabu ya SoNy Sugar itaondolewa katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) iwapo itakosa kufika Moi Stadium kucheza leo Jumamosi saa sita kucheza na majirani wake Kisumu All Stars.

Tayari klabu hiyo ya Awendo imekosa kufika uwanjani mara mbili mfululizo kucheza na AFC Leopards kwao Awendo na baadaye ikakosa kusafiri kucheza na Bandari katika mechi ambayo iliratibiwa kuchezewa Mbaraki Stadium, Mombasa.

Kulingana na Afisa Mkuu wa kampuni ya KPL inayosimamia mechi hizo, hii itakuwa mara ya tatu ambapo kulingana na sheria hiyo itakuwa mara ya mwisho na itateremshwa ngazi hadi daraja la pili (Supa Ligi).

Kulingana na sheria za KPL, tayari SoNy itatozwa jumla ya Sh1.5 milioni kwa kukosa kufika uwanjani mara mbili.

Huenda matatizo ya kifedha yakasababisha kutofika uwanjani kwa timu kadhaa za soka wikendi hii kucheza mechi baada ya KPL kusisitiza kwamba zitaendelea kama zilivyopangwa.

Timu kadhaa zilikuwa zimetoa vilio zikitaka ligi hiyo ipigwe breki baada ya kujiondoa ghafla kwa wadhamini SportPesa.

Oguda alisema kwamba kufikia sasa, wamezungumza na mashirika mbalimbali, lakini kutokana na hali mbaya ya uchumi nchini, ofa wanazotoa haziwezi kukidhi mahitaji ya ligi hiyo kikamilifu.

Kulingana na taarifa yake, huenda ikachukua muda kurasmisha udhamini wowote kwa sababu mashirika mengi tayari yanaenda na bajeti mpya ya 2019/2020 ambayo iliidhinishwa rasmi mwezi Juni.

Oguda kadhalika alitoa mwito kwa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) litumie uwezo wake kutafuta njia nyingine za kuokoa timu ambazo zinazidi kuumia kutokana na uchumi mbaya unaokabilia taifa kwa jumla.

Ratiba leo (Jumamosi): SoNy Sugar na Kisumu All Stars (Moi Stadium, Kisumu), Nzoia Sugar na Kariobangi Sharks (Sudi, saa tisa), Chemelil Sugar na Kakamega Homeboyz (Chemelil, saa tisa), Ulinzi Stars na Tusker FC (Afraha Stadium, saa tisa), KCB na Zoo Kericho (Kericho Green Stadium, saa tisa), Posta Rangers na Wazito (saa nane). Kesho: Sofapaka na AFC Leopards (Narok, saa kumi na robo).