Michezo

SoNy Sugar yatimua wachezaji 4 licha ya kuburuta mkia ligini

May 24th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya SoNy Sugar inayovuta mkia katika msimamo wa jedwali la ligi ya KPL imeamua kuwatema wachezaji wake wanne kabla hata mkondo wa kwanza wa ligi kukamilika.

Wanne hao ni Kiungo Jesse Obare na Kelvin Muhanji huku wengine wakiwa ni kipa Kevin Olang’o na mchezaji wa pembeni Tyron Owino.

Wachezaji Muhanji na Owino walijiunga na klabu hiyo mwezi Januari mwaka huu kutoka timu za Vihiga United na Bandari mtawalia.

Hata hivyo imebainika kwamba sababu kuu ya kutemwa kwa wanne hao ilitokana na utovu wa nidhamu na kushuka kwa viwango vyao vya kutandaza gozi.

“Tumetimuliwa bila kupewa maelezo. Nimekuwa nikitia bidii katika mazoezi na wakati wa mechi na uamuzi huo wa klabu umenishangaza mno. Sasa natafuta klabu nyingine ya kusakatia,” akasema mchezaji moja aliyeangukiwa na shoka hilo.

Pia ripoti zilizothibitishwa zinaeleza kwamba baadhi ya wachezaji katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo wanatumikia marufuku ya kutoshirikishwa kwenye mechi za ligi.

Wachezaji Yema Mwana, Benjamin Mwosha, Victor Ademba na David Simiyu wote wamepigwa marufuku ya kutoshirikishwa katika kikosi cha kwanza kwa muda usiojulikana.

SoNy ambao waliutwaa ubingwa wa KPL mwaka wa 2006 wamekuwa na msimu mbovu na wasipojiimarisha kupitia ushindi wa mechi zake zijazo, klabu haitakuwa na jingine ila kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu.

Baada ya kushiriki mechi 15, SoNy wanakokota nanga katika jedwali wakiwa wamesajili alama 11 pekee.

Wanasukari hao hawajaandikisha ushindi wowote tangu walipoanza ligi kwa matao ya juu kwa kushinda mechi zake mbili dhidi ya Klabu za Ulinzi na Zoo Kericho licha ya kupoteza mechi ya ufunguzi dhidi ya Wazito FC.

Licha ya kumleta kocha mpya Patrick Odhiambo kutoka kwa majirani zao Chemelil FC baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa kocha wao Salim Babu mambo hayaonekani kubadilika.