Michezo

Sony yaramba Ulinzi kwenye ligi kuu ingawa kwa jasho kuu

February 12th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Kwa Muhtasari:

  • Kevin Omondi alisukuma wavuni bao la pekee dakika ya 16
  • Kariobangi Sharks ilikabwa 2-2 na wageni Vihiga United uwanjani Machakos
  • Mechi kati ya mabingwa mara 11 Tusker na wageni wao Posta Rangers ilimalizika 0-0 uwanjani Ruaraka

SONY Sugar iliendelea kuonyesha Ulinzi Stars kivumbi ilipoilaza bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL) uwanjani Awendo Jumapili.

Kevin Omondi alisukuma wavuni bao hilo muhimu dakika ya 16. Wanasukari wa SoNy, ambao walishinda ligi mwaka 2006, walibahatika kumaliza mechi hiyo na pointi zote tatu hasa baada ya mchezaji wake Yemi Mwana kulishwa kadi nyekundu katika dakika ya 90.

Rekodi ya SoNy kutopigwa na mabingwa mara nne Ulinzi sasa imefika mechi nane. Timu hizi zilikuwa zimetoka sare mara nne mfululizo kabla ya SoNy kuandikisha ushindi wake wa kwanza msimu huu. Ilizabwa 1-0 na Wazito katika mechi ya kwanza, ambayo SoNy pia ilimaliza watu 10 uwanjani baada ya Benard Omondi kuonyeshwa kadi nyekundu.

Katika mechi iliyopigwa mapema Jumapili, Kariobangi Sharks ilikabwa 2-2 na wageni Vihiga United uwanjani Machakos. Timu hizi zilimaliza kipindi cha kwanza bila kufungana kabla ya Vihiga kupata bao la ufunguzi dakika ya 47 kupitia Andrew Murunga.

Sharks ilisawazisha kupitia raia wa Gambia Ebrimah Sanneh dakika ya 52 kabla ya kuongoza 2-1 kupitia bao la Eric Kapaito dakika nne baadaye.

Hata hivyo, Vihiga haikuwa tayari kupokea kichapo cha pili mfululizo na ikajikakamua na kusawazisha 2-2 kupitia Murunga dakika ya 63.

Vihiga, ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kabisa ilianza msimu kwa kulimwa 2-1 na Mathare United wiki moja iliyopita uwanjani Bukhungu. Sharks, ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa mwaka wa pili mfululizo, ilifungua msimu huu kwa kupiga Nzoia Sugar 1-0.

Mechi kati ya mabingwa mara 11 Tusker na wageni wao Posta Rangers ilimalizika 0-0 uwanjani Ruaraka. Klabu zote mbili hazina ushindi msimu huu.

Tusker ilipoteza 2-0 dhidi ya Chemelil Sugar katika mechi ya ufunguzi nayo Rangers ikagawana pointi baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya AFC Leopards. Tukienda mitamboni Nzoia ilikuwa bao 1-1 dhidi ya wenyeji wake Mathare United.

Bao la George Mutimba lilipatikana dakika ya 31 naye Chrispin Oduor akasawazisha.