Habari Mseto

Sossion apata fursa ya kuponda Magoha kwenye kizaazaa

August 9th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIZAAZAA kilizuka Alhamisi kwenye kikao cha Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu baada ya Waziri wa Elimu Prof George Magoha kujibizana vikali na Mbunge Maalum Bw Wilson Sossion.

Bw Sossion, ambaye ni mwachama wa kamati hiyo, alimtaka Prof Magoha kueleza mikakati ambayo wizara yake imeweka ili kukabili ukosefu wa usalama katika shule za msingi katika wadi ya Kiunga Mashariki katika Kaunti ya Lamu.

Kikao hicho kilikuwa kikiendelea katika Ukumbi wa County Hall, jijini Nairobi, ambapo waziri huyo alikuwa akiieleza kamati hiyo kuhusu hali ya elimu nchini.

Swali hilo lilikuwa limeulizwa na Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruveida Obo, ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo, akilalama kuwa hali hiyo imeathiri shughuli za masomo katika karibu shule zote za wadi hiyo.

“Ningemtaka waziri kuelezea hatua ambazo serikali inachukua kuimarisha usalama katika shule hizo, kwani hakuna shughuli za masomo ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka minnne kufikia sasa,” akauliza Bi Obo.

Mbunge huyo alisema kuwa wale ambao wameathiriwa sana na hali hiyo ni watu wa jamii ya Waboni, aliodai idadi yao ni chini ya 1,000 kote nchini.

Alipoelekezewa swali hilo, Prof Magoha alisema kuwa hawezi kulijibu, kwani suala la usalama wa taasisi zozote, hata zile za elimu ni jukumu la Wizara ya Usalama wa Ndani.

“Ndugu Mwenyekiti (Sossion) naomba kutojibu swali hilo, kwani hilo si jukumu langu. Kuna maafisa wa usalama na ujasusi ambao wako katika eneo hilo lakini huwa hawaripoti kwangu. Hivyo siwezi kulijibu swali hilo,” akasema Prof Magoha.

Hata hivyo, Bi Obo alilalamika, akimtaka huyo waziri kufafanua zaidi, kwani hali ya usalama katika maeneo yanayopakana na wadi hiyo hayana matatizo yoyote ya kiusalama.

“Ningemtaka waziri kutufafanulia zaidi, kwani wadi jirani ya Basuba haina tatizo hilo. Walimu huwa wanatoka katika eneo hilo kuja katika wadi ya Kiunga kwa shughuli za kimasomo, lakini huwa wanarejea makwao. Ningemtaka kueleza mbona hali ni tofauti katika wadi hizo mbili zinazopakana,” akarai mbunge huyo.

Akionekana kumuunga mkono Bi Obo, Bw Sossion alimshinikiza waziri kutoa ufafanuzi kamili kuhusu inavyofanya wizara yake, akisema kuwa duniani kote, jukumu la usalama wa taasisi za elimu huendeshwa na wizara hiyo.

Bw Sossion pia aliungwa mkono na Mbunge Mwanamke wa Kaunti ya Migori, Dkt Rosemary Odhiambo, ambaye pia alimrai Prof Magoha kueleza wizara inavyofanya.

Waziri alipandwa na mori, akisisitiza kuwa hatajirudia. “Siwezi kurudi kwa swali hilo!” akafoka Prof Magoha.

Akionekana kuridhika, japo shingo upande, Bw Sossion alimrai Bi Odi kutafuta ufafanuzi zaidi kutoka kwa wizara za elimu na usalama wa ndani kuhusu yule anayepaswa kusimamia usalama.

Kwa kuona hali ilivyokuwa, Bw Sossion aliamua kuendelea na maswali mengine.

Wadau mbalimbali wa elimu wamekuwa wakilalamika kuwa imekuwa vigumu kufikia misimamo ya pamoja na waziri huyo, wakimtaja kutekeleza yale anayoamini yanafaa.