Michezo

South B United, Acakoro Ladies ndani ya fainali Chapa Dimba

April 29th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya South B United na Acakoro Ladies zimeibuka wafalme na malkia wa kinyang’anyiro cha Chapa Dimba na Safaricom Season Two katika Mkoa wa Nairobi msimu huu.

Licha ya kubanduliwa katika fainali na Gor Mahia Youth mwaka 2018, South B United ilivuna ushindi huo ilipozaba Jericho Allstars kwa mabao 2-1 katika fainali ya kusisimua iliyosakatiwa Uwanja wa Taasisi ya Goan Pangani, Nairobi.

Nayo Acakaro Ladies ya kocha, Pauline Awuor ilihifadhi umalkia wa kipute hicho ilifanikiwa kukomoa Carolina for Kibera kwa magoli 5-4 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

Janet Ajiambo wa Acakoro Ladies (mbele) akishindana na Pauline Akoth wa Carolina for Kibera katika fainali ya wasichana kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two Mkoani Nairobi iliyopigiwa uwanja wa Taasisi ya Goan Pangani, Nairobi. Acakoro Ladies ilishinda kwa mabao 5-4 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. Picha/ John Kimwere

Kwa wavulana Fabio Otieno aliiweka Jericho Allstars kifua mbele dakika ya 27, kabla ya South B United kufanya kweli kupitia Alvin Kuka na Meshack Omondi waliotinga bao moja kila mmoja.

”Tuna furaha kuibuka washindi na kufuzu kucheza fainali za kitaifa mwaka huu,” kocha wa South B United, John Mandela alisema.

Katika muda wa kawaida kitengo cha wasichana, Catherine Awuor aliitingia Acakoro Ladies kabla ya Carolina for Kibera kusawazisha kupitia Pauline Nyanduko.

Juma Michael wa Jericho Allstars (kulia) akijaribu kumzuia mpinzani wake Meshack Omondi wa South B United katika fainali ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two Mkoani Nairobi iliyopigiwa uwanja wa Taasisi ya Goan Pangani, Nairobi. South B United ilishinda mabao 2-1. Picha/ John Kimwere

Mafanikio hayo yalifanya South B United na Acakoro Ladies kila moja kunasa tiketi ya kusonga mbele kugaragaza fainali za kitaifa zitakazoandaliwa kule Kinoru Stadium katika Kaunti ya Meru mwezi Juni mwaka huu.

Kwenye nusu fainali, South B United ili ya kocha, John Mandela iliicharaza Uweza FC mabao 2-0 nayo Jericho Allstars ilibeba mabao 2-1 dhidi ya Brightstar Academy.

Carolina for Kibera ilishinda Dagorettti Mixed mabao 4-3 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare tasa. Acakoro Ladies ilizima County Queens kwa magoli 4-1 kwa mabao 4-1.

Mfungaji bora wa kiume Bramwell Kavaya wa Jericho Allstars atuzwa. Picha/ John Kimwere

Mabingwa hao kila moja ilipoeka Sh200,000 huku wachezaji nao kila mmoja akipongezwa kwa simu ya dhamani ya Sh10,000.

Licha ya wapinzani wao, Jericho Allstars na Carolina for Kibera kumaliza nafasi ya pili kwa wavulana na wasichana mtawalia kila moja ilipokea zawadi ya Sh100,000 kujipangusa vumbi kwa kujitahidi na kutinga hatua hiyo.

WACHEZAJI BORA WATUZWA

Bramwell Kavaya wa Jericho Allstars kitengo cha wavulana alipokea tuzo ya mfungaji bora, huku ikiwaendea wasichana wawili waliofunga mabao mawili kila moja, Sylvia Makhungu na Catherine Awuor wote Acakoro Ladies.

Wafungaji bora wa kike Sylvia Makhungu na Catherine Awuor wote Acakoro Ladies wapokea tuzo. Picha/ John Kimwere

Nao Enock Wanyama (South B United) na Hashina Diana (Acakoro Ladies) walituzwa nyota bora kwa wavulana na wasichana mtawalia. Kipa bora wavulana aliibuka Caleb Omondi(Jericho Allstars) na Yvonne Adhiambo wa Acakoro Ladies. Chipukizi hao kila mmoja alituzwa Sh30,000.

”Tunashukuru kuibuka mabingwa baada ya kushindwa na Gor Mahia Youth mwaka uliyopita,” kocha wa South B United alisema. Naye nyota bora kwa wavulana, Enock Wanyama alisema ”Nahisi vizuri ambapo nataka kusonga mbele ambapo nikibahatika kushiriki soka la kulipwa sitawahi kusahau timu yangu mtaani.”

Mchezaji bora wa kike Hashina Diana (Acakoro Ladies). Picha/ John Kimwere

Mchezaji huyo aliibuka kati ya walioteuliwa katika timu ya taifa inayotazamiwa kwenda Uhispania mapema wiki lijalo kushiriki maozezi dhidi ya baadhi ya vikosi vya kipute cha La Liga.

”Kiukweli Carolina for Kibera haikuwa mteremko jinsi ilitupatia shughuli zito kinyume na tulivyotarajia,” mlinda lango wa Acakoro Ladies, Yvonne Adhiambo alisema.

Mwanasoka bora wa kiume Enock Wanyama (South B United) apokea zawadi. Picha/ John Kimwere

”Tunashukuru Safaricom inafanya kazi nzuri kukuza wachezaji chipukizi maana soka ni ajira inayolisha wengi duniani,” ofisa mkuu FKF Nairobi West, Bashir Hussein alisema na kutoa mwito kwa mashirika mengine yajitokeze kupiga jeki sekta ya spoti nchini.

Mabingwa hao wamejiunga na wenzao kutoka Mikoa mingine ikiwamo: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa), wavulana wa Berlin (Kaskazini Mashariki) pia wavulana wa Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati).

Kipa bora wa kike Yvonne Adhiambo wa Acakoro Ladies apokezwa zawadi. Picha/ John Kimwere