Michezo

Southampton raha tele baada ya kuongoza jedwali la EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32

November 7th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Ralph Hasenhuttl wa Southampton amewaambia wanasoka wake kwamba “chochote kinawazekana” katika ulingo wa kabumbu baada ya kikosi chake kupiga Newcastle United 2-0 uwanjani St Mary’s na kuongoza jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza tangu 1988.

Southampton walisajili ushindi huo mwaka mmoja tangu wadhalilishwe 9-0 na Leicester City katika kichapo ambacho kiliweka Hasenhuttl ambaye ni raia wa Austria kwenye hatari ya kufutwa kazi.

“Mashabiki wetu wanapendezwa na hali ya sasa ya Southampton. Huu kwetu ni ufanisi mkubwa ambao unastahili kutuinua zaidi na kuchangia motisha ambayo itatukweza pazuri mwishoni mwa kampeni za msimu huu,” akasema mkufunzi huyo.

Huku Southampton wakipaa kileleni mwa jedwali kwa alama 16 sawa na mabingwa watetezi Liverpool, Newcastle walishuka hadi nafasi ya 11 kwa alama 11 sawa na Manchester City ambao watakuwa wenyeji wa Liverpool ugani Etihad mnamo Novemba 8, 2020.

“Tulizembea na kutepetea katika safu zote. Wenyeji walituzidi maarifa kuanzia dakika ya kwanza na ikawa vigumu kurejea mchezoni baada ya kufunga mabao mawili,” akasema kocha Steve Bruce wa Newcastle United almaarufu The Magpies.

Kutokuwepo kwa mshambuliaji Danny Ings kwa upande wa Southampton kwenye mchuano huo kulimpa Che Adams fursa ya kuendeleza ubabe wake kwa kufunga bao kunako dakika ya saba kabla ya kuchangia la pili lililojazwa wavuni na Staurt Armstrong katika dakika ya 82.

Newcastle kwa sasa wamefungwa bao katika kila mojawapo ya mechi saba zilizopita, kipindi hicho kikiwa kirefu zaidi kwa kikosi kutokamilisha mechi bila ya kufungwa tangu Disemba 2017.

Kwa upande wao, Southampton wameshinda mechi zao zote tatu zilizopita ligini kwa mara ya kwanza tangu waibuke washindi wa michuano minne iliyopita mfululizo tangu Mei 2016 chini ya kocha Ronald Koeman.

Southampton watarejea uwanjani baada ya likizo fupi itakayopisha mechi za kimataifa kuvaana na Wolves uwanjani Molineux huku Newcastle wakiwaalika Chelsea mnamo Novemba 21, 2020.